TAKUKURU yaokoa shilingi bilioni 1.4 za Manispaa ya Kibaha

PWANI-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imeokoa zaidi ya shilingi bilioni 1.4 za Manispaa ya Kibaha zilizopotea kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kutokuwa tayari kulipa ushuru wa huduma.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani,Domina Mukama ametoa taarifa hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba,2025.

Amesema kuwa,TAKUKURU ilifanya uzuiaji katika ukusanyaji wa mapato upande wa ushuru wa huduma katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha na kufanikiwa kukusanya kiasi hicho cha fedha cha Sh.bilioni 1.4.

Mukama amesema,katika ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato hayo Takukuru ilibaini mambo mbalimbali ikiwemo baadhi ya wafanyabiashara kuwapangisha wafanyabiashara wenzao hali iliyosababisha waliopangishwa kutolipa ushuru wa huduma kulingana na Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Manispaa ya Kibaha.

Amesema,baadhi ya wafanyabiashara vituo vya nishati ya mafuta (Petrol Station) kuuza nishati hiyo nje ya mfumo wa TRA kwa kutumia madumu yenye ujazo wa lita tano hadi ishirini hali ambayo ilikuwa inasababisha upotevu wa mapato.

Amesema, pia baadhi ya wafanyabiashara kumiliki viwanda vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, lakini vimesajiliwa mikoa mingine na kuleta mkanganyiko kwa wawekezaji kujua sehemu sahihi ya kulipa ushuru wa huduma.

Mukama ameongeza kuwa,baadhi ya wafanyabiashara wanapotaka kulipa ushuru wa huduma wanajikadiria mauzo yao hivyo kusababisha kulipa ushuru wa huduma kiasi kidogo ukilinganisha na mauzo halisi kutoka kwenye mfumo wa Z-Report kama Sheria inavyowataka .

Amesema,jambo lingine walilolibaini katika ufuatiliaji huo ni pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kulipa nusu au kutokulipa kabisa ushuru wa huduma kwa madai kwamba Kibaha ni eneo la uzalishaji wa viwanda na sio eneo la mauzo na wengine kumiliki mashine za ukusanyaji ushuru (EFD mashine)zaidi ya moja na hivyo kuficha zingine ili kukwepa kulipa ushuru.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here