Tanzania inaunga mkono juhudi za kurejesha utulivu Sudan na kulinda umoja wa Somalia-Waziri Kombo

ADDIS ABABA-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amesema Tanzania inaunga mkono juhudi za kurejesha utulivu Sudan na kulinda umoja Somalia na kwamba kuna haja ya kuendelea kuzungumza kwa sauti moja katika masuala yanayogusa mamlaka ya pamoja, utulivu na mustakabali wa bara la Afrika.
Balozi Kombo amesema hayo alipozungumza wakati wa Mkutano wa Umoja wa Afrika wa Mawaziri wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kuhusu hali ya Sudan na Somalia unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Mhe. Kombo amepongeza kitendo cha Serikali ya Mpito ya Sudan kurejea jijini Khartoum, na kuongeza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika safari ya taifa hilo ya kurejesha mamlaka ya dola na kuanza upya ujenzi wa nchi baada ya miaka ya mgogoro.
Balozi Kombo amesema, kurejea kwa Serikali Sudan ni ishara ya matumaini kwa wananchi ambayo itasaidia kurejesha hali ya kawaida na kuanzisha upya ujenzi wa mji mkuu na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuisaidia Sudan katika kuendeleza mazungumzo jumuishi yanayoongozwa na Wasudan wenyewe, akisisitiza kuwa mchakato huo wa kisiasa ndio msingi wa kufikia utulivu wa kudumu.

“Tunasisitiza umuhimu wa mazungumzo jumuishi yanayomilikiwa na Wasudan wenyewe kama njia pekee ya kufanikisha amani ya kudumu na utulivu wa kisiasa nchini humo,”amesema Balozi Kombo.

Kuhusu Somalia, Balozi Kombo amesisitiza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaunga mkono kikamilifu Jamhuri ya Shirikisho la Somalia na inapinga vikali hatua zozote zinazoweza kudhoofisha au kugawanya eneo hilo na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu umoja, mamlaka kamili ya nchi, uadilifu wa mipaka na uhuru wa kisiasa wa Somalia kwa mujibu wa Katiba yake ya Mpito, Hati ya Umoja wa Afrika na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Ameongeza kuwa, ni jukumu la wananchi wa Somalia kuamua mfumo wa utawala unaolinda maslahi ya sehemu zote za nchi yao na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuunga mkono juhudi za kuleta utulivu nchini humo na kuepuka hatua zinazoweza kuhatarisha umoja wake.

Amesema, Afrika inapitia kipindi nyeti katika mazingira ya siasa za kimataifa yanayobadilika kwa kasi, hali inayohitaji kuimarishwa kwa umoja na mshikamano miongoni mwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika na kuongeza kuwa ushirikiano wa pamoja ni muhimu katika kulinda mamlaka ya dola, kuendeleza Ajenda 2063 na kushughulikia kwa ufanisi changamoto za kikanda.
“Ni lazima tuendelee kuzungumza kwa sauti moja katika masuala yanayogusa mamlaka yetu ya pamoja, utulivu na mustakabali wa bara letu,” amesisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here