Tanzania yafungua fursa biashara ya mbolea

DAR-Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kufungua fursa ya biashara ya mbolea nchini, kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo katika mkutano wa kimataifa wa wadau wa mbolea barani Afrika-ARGUS, unaoendelea jijini Dar es salaam.
Akimwakilisha Waziri wa Kilimo,Mheshimiwa Daniel Chongolo, mgeni rasmi wa mkutano huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula), Prof. Peter Msofe amesema, Tanzania imejipanga kuhakikisha sekta ya mbolea nchini inaimarika kwa manufaa ya wakulima na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Profesa Msofe amesema kuwa,mbolea ni nyenzo ya kimkakati katika kufanikisha usalama wa chakula, kuongeza uzalishaji wa mazao na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ameongeza kuwa,Tanzania inaendelea kutoa vipaumbele vya kikanda na Bara ikiwemo Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (CAADP), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA),Joel Laurent amesema, Tanzania ni miongoni mwa masoko ya mbolea yanayokua kwa kasi zaidi barani Afrika, na kuchochea matumizi ya mbolea kutoka tani 360,000 mwaka 2021/2022 hadi takribani tani milioni moja kwa mwaka 2024/2025, huku matarajio yakionesha mahitaji kufikia tani milioni 2.1 ifikapo mwaka 2030.
Laurent ameongeza kuwa, utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea kwa Njia ya Kidijitali umeongeza upatikanaji wa mbolea huku juhudi za Serikali zikijikita katika kukuza uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi, kupitia uwekezaji katika viwanda, matumizi ya malighafi zilizopo na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ubora wa mbolea.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wadau wa mbolea nchini waliohudhuria mkutano huo, wamesema kuwa wamepata fursa kukutana na wadau wengine wa mbolea duniani na kubadilishana uzoefu katika biashara hiyo, jambo litakalochochea ukuaji wa biashara ya mbolea nchini.
Mkutano wa Mbolea Afrika Argus 2026 unawakutanisha watunga sera, wawekezaji, wasafirishaji, wazalishaji na wadau wa sekta ya mbolea kutoka Afrika na nje ya bara, ukilenga kujadili fursa za uwekezaji, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuweka mikakati, kuhakikisha upatikanaji wa mbolea bora na kwa gharama nafuu ili kuchochea maendeleo ya kilimo na usalama wa chakula.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here