ZANZIBAR-Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imefanya ziara ya kikazi katika Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo (KUMM) Zanzibar kwa lengo la kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za usimamizi na udhibiti wa mbolea kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, hatua inayolenga kuongeza tija ya uzalishaji wa kilimo na kuboresha maisha ya wakulima.
Akizungumza wakati wa ziara Februari 2, 2026,Naibu Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Dkt. Salum Soud Hamed,alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na TFRA katika kuhakikisha wakulima wanapata mbolea bora, jambo litakalowawezesha kuongeza uzalishaji, kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo Zanzibar.
Aidha, Dkt.Salum alisisitiza kuingia Makubaliano ya Kiutendaji ( MoU) baina ya TFRA na Wizara ya Kilimo Zanzibar yatakayo boresha na kuimarisha mahusiano ya kiutendaji kwa maslahi mapana ya kuinua uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent amesema kuwa, ushirikiano wa karibu kati ya TFRA na Wizara ya Kilimo Zanzibar ni muhimu katika kuhakikisha wakulima wanapata mbolea yenye ubora unaokubalika na kwa wakati.
Aidha, Joel amesisitiza kuwa, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya udhibiti kutasaidia kuongeza ufanisi katika kusimamia tasnia ya mbolea, kulinda maslahi ya wakulima na kuchangia kukuza uzalishaji wa kilimo pamoja na usalama wa chakula nchini.








