NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa mvua za Masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2026, ikieleza kuwa maeneo mengi ya pwani ya kaskazini na baadhi ya ukanda wa Ziwa Victoria yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, huku nyanda za juu kaskazini mashariki zikitabiriwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Hayo yamebainishwa leo Februari 5,2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),Dkt.Ladislaus Chang'a wakati akitoa mwelekeo huo kwa waandishi wa habari.
Dkt.Ladislaus Chang'a ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) amesema, msimu wa mvua za Masika ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki inayojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Pwani ya kaskazini ambayo inajumuisha kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mkoa wa Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Vilevile,ukanda wa Ziwa Victoria unaojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
Dkt.Chang'a amesema,mvua za Masika zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Februari hadi wiki ya kwanza ya mwezi Machi,2026 katika ukanda wa Ziwa Victoria, na wiki ya kwanza hadi ya pili ya mwezi Machi,2026 katika maeneo ya pwani ya kaskazini.
Wiki ya pili hadi ya tatu ya mwezi Machi itakuwa ni katika nyanda za juu kaskazini mashariki ambapo mvua hizo zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya nne ya mwezi Mei na wiki ya kwanza ya mwezi Juni, 2026, huku ongezeko la mvua likitarajiwa zaidi mwezi Aprili,2026.
"Kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa katika kipindi cha Masika, mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya pwani ya kaskazini pamoja na baadhi ya maeneo ya magharibi mwa ukanda wa Ziwa Viktoria hususani mikoa ya Kagera, Geita na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
"Aidha, mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria hususani mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu. Ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Aprili, 2026."
Mbali na hayo, amebainisha kuwa matukio ya hali mbaya ya hewa, ikiwemo mvua kubwa za muda mfupi, yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotabiriwa kupata mvua za chini ya wastani.
Dkt. Ladislaus Chang'a ameeleza kuwa, kutokana na mvua hizo zinaweza kusababisha athari za mafuriko na unyevu kupita kiasi mashambani, uharibifu wa miundombinu,kuenea kwa magonjwa ya mimea, mifugo na binadamu.
Aidha, amesema zinaweza kusababisha changamoto katika sekta ya usafiri, ujenzi na maji huku maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chache yanaweza kukumbwa na upungufu wa maji kwa matumizi ya nyumbani, kilimo na mifugo.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo imetoa ushauri mahsusi kwa sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Kilimo ambapo wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba kwa wakati, kutumia mbinu za kuhifadhi maji, kudhibiti magonjwa na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani.
Dkt.Chang'a amesema, kwa upande wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi, wafugaji wanatakiwa kupanga matumizi ya maji na malisho, na kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mifugo.
Upande wa Sekta ya Usafiri na Ujenzi, wadau wameshauriwa kufuatilia utabiri wa kila siku ili kupunguza athari za mafuriko na kuchelewa kwa miradi.
Aidha, kwa upande wa Sekta ya Afya, jamii zimetakiwa kutumia maji safi na salama na kuchukua hatua za kudhibiti magonjwa ya mlipuko yanayohusiana na maji na wadudu.
Pia, upande wa Serikali za Mitaa, zimehimizwa kuimarisha mifumo ya maji, mifereji ya maji ya mvua na mipango ya kudhibiti maafa.
TMA imesisitiza kuwa,mwelekeo huu ni wa jumla kwa msimu mzima, hivyo wananchi na wadau wanahimizwa kuendelea kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 na mwezi pamoja na tahadhari rasmi zitakazotolewa mara kwa mara.
“Matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa ni msingi muhimu wa kulinda maisha, mali na kukuza uchumi,” ameongeza.
Awali, akizungumzia kuhusu mwenendo wa mvua za Msimu kuanzia Novemba, 2025 hadi Aprili, 2026 amesema kuwa,mvua hizo ambazo utabiri wake ulitolewa mwezi Oktoba, 2025 zilitarajiwa kuwa za Chini ya Wastani hadi Wastani katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida na Dodoma.
Aidha, mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zilitarajiwa katika mikoa Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Mtwara, Lindi, pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro.
"Mvua hizi zilianza mapema wiki ya nne ya Oktoba na wiki ya kwanza ya Novemba, 2025 katika maeneo mengi ya Magharibi mwa nchi na kufuatiwa na maeneo ya nyanda za juu kusini magharibi wiki ya pili ya mwezi Novemba kama ilivyotabiriwa.
"Aidha, ongezeko la mvua lilijitokeza zaidi mwezi Desemba, 2025 katika maeneo mengi. Katika kipindi kilichosalia cha msimu (Februari hadi Aprili, 2026) mvua zinatarajiwa kuendelea kama ilivyotabiriwa."
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Mvua za Masika
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania


