Uber yasitisha tena kutoa huduma Tanzania

NA DIRAMAKINI

KAMPUNI ya usafiri wa teksi mtandaoni ya Uber Technologies, Inc. (Uber) imesitisha kutoa huduma za usafiri nchini Tanzania baada ya kuhudumia soko hilo kwa miaka kadhaa.
Awali kampuni hiyo yenye makao yake makuu mjini Amsterdam, Uholanzi iliwafahamisha wateja wake kuwa huduma zake zilikoma Januari 30,2026 nchini Tanzania.

Katika ujumbe uliotumwa kwa watumiaji, Uber ilisema kuwa mfumo wake wa programu tumishi (app) hautapatikana tena nchini Tanzania, huku ikiomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza na kuwashukuru wateja kwa msaada wao kwa miaka yote hiyo.

“Sura hii inafikia kikomo, lakini shukrani zetu kwenu zinabaki,” ilisema kampuni hiyo, bila kutoa maelezo ya kina hadharani kuhusu sababu zilizopelekea uamuzi huo.

Uber iliingia Tanzania kwa mara ya kwanza Juni, 2016, ikizindua huduma zake jijini Dar es Salaam kama sehemu ya upanuzi wake mkubwa katika miji ya Afrika.

Awali, mfumo huo ulipokelewa vyema kwa kuanzisha usafiri wa teksi kwa njia ya programu, malipo yasiyohusisha fedha taslimu, na bei zenye ushindani, hususani miongoni mwa wasafiri wa mijini.

Aprili 2022, kampuni hiyo ilisitisha operesheni zake baada ya serikali kuanzisha kanuni mpya, zikiwemo ukomo wa nauli na makato ya kamisheni.

Aidha,ilirejea kutoa huduma mapema mwaka 2023 kufuatia maboresho katika mfumo wake wa biashara, lakini ushindani kutoka kwa mifumo ya ndani na ya kikanda, pamoja na shinikizo za kikanuni zinazoendelea, viliendelea kuathiri soko hilo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mahusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini nchini (LATRA), Salum Pazzy amesema,taarifa zilizokuwa zikisambaa kuwa Uber imejiondoa nchini ni sahihi na wamepokea barua rasmi.

“Ni kweli kumekuwa na taarifa mbalimbali za Uber kujiondoa nchini, na sisi mamlaka ya udhibiti tunathibitisha kampuni hiyo imesitisha huduma kwa muda, si kujiondoa moja kwa moja,” amesema Pazzy.

LATRA ilipokea barua ya kampuni hiyo, iliyoandikwa Januari 30, 2026, kutoka ofisi za Uber BV zilizopo Amsterdam, Uholanzi ikieleza uamuzi wa kusitisha huduma kwa muda katika soko la Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here