ARUSHA-Wataalamu wa Kamisheni ya Kudumu ya Pamoja ya Ulinzi na Usalama (JPCDS-Joint Permanent Commission on Defence and Security) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia wametakiwa kuendelea kuimarisha mwelekeo wa pamoja na kuweka msingi thabiti wa maamuzi na mashirikiano yatakayoleta manufaa ya moja kwa moja kwa nchi zote mbili. 

Wito huo unalenga kuhakikisha kuwa ushirikiano huo unaendelea kuleta amani, usalama na ustawi si tu kwa mataifa hayo mawili bali pia kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Bara la Afrika kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ally S.Gugu, Februari 25, 2025, wakati akifunga kikao cha nne cha JPCDS kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Arusha International Conference Centre (AICC) jijini Arusha.
Kikao hicho kilihusisha Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta za Ulinzi,Mambo ya Ndani.Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi za nchi hizo mbili ambao walipokea taarifa na mapendekezo kutoka kwa Wataalamu wa Kamisheni ya Pamoja ya Kudumu ya Sekta za Ulinzi na Usalama baada ya kikao chao cha jana Februari 24,2026.
Amesisitiza kuwa, kikao hicho kimeweka msingi imara wa kuendeleza ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Zambia katika masuala ya ulinzi na usalama.
Aidha, Mhe. Gugu ameeleza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika sekta za kimkakati kama vile Ulinzi na Usalama ili kudhibiti kwa ufanisi uhalifu unaovuka mipaka na matishio mengine ya kiusalama.
Mhe. Gugu amesema wataalamu wameandaa mapendekezo yenye tija ambayo yamepitiwa, kuboreshwa na kupitishwa, na kwamba wana imani Mawaziri wa nchi hizo mbili watayapokea kwa uzito unaostahili na kuyatumia kama msingi wa maamuzi yatakayowanufaisha wananchi wa mataifa yote mawili.
Kumalizika kwa mkutano huo ni maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa JPCDS utakaofanyika Februari 27, 2026, jijini Arusha. Lengo la mkutano huo ni kujadiliana,kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ushirikiano na kuongeza juhudi za pamoja.














