DODOMA-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ametoa pole kwa Bi Elizabeth Molel, ambaye ni mjane wa marehemu Edwin Emanuel Nalaila aliyekuwa mtumishi wa Wizara ya Fedha aliyefariki dunia Februari 5, 2026 jijini Dodoma.
Mhe. Balozi Omar alitoa salamu hizo za pole alipofika nyumbani kwa marehemu Makulu Oysterbay jijini Dodoma, akiambata na Naibu Waziri wake, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), kuungana na waombolezaji wengine akieleza kuwa, marehemu alikuwa sehemu ya watumishi wa Wizara waliotoa mchango mkubwa wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Mhe. Balozi Omar alisema,Wizara itaendelea kushirikiana na familia ya marehemu ili kuhakikisha kuwa shughuli za kumpumzisha marehemu zinakamilika kikamilifu.
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alitoa pole kwa familia ya Marehemu Edwin Emanuel Nalaila na kueleza kuwa marehemu alikuwa mchapakazi hodari na kuwa Wizara itaendelea kumkumbuka kwa utumishi wake.
Marehemu Edwin Emanuel Nalaila alikuwa Afisa Tehama Mwandamizi katika Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Fedha na Huduma za Ndani za TEHAMA, alifariki katika hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma tarehe 5 Februari 2026 wakati akipatiwa a matibabu na anatarajiwa kuzikwa mkoani Arusha.





