Zanzibar ni mahali sahihi pa kuwekeza,Rais Dkt.Mwinyi awaeleza Wafaransa

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameyakaribisha makampuni na wawekezaji kutoka nchini Ufaransa kuja kuwekeza Zanzibar, hususan katika sekta kuu za uchumi ikiwemo utalii, akieleza kuwa Zanzibar iko tayari kupokea uwekezaji wenye tija na endelevu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Februari 27,2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Bi.Anne Sophie, aliyefika kwa mazungumzo ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Zanzibar na Ufaransa.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji wawekezaji makini na wenye mitaji ya kutosha watakaowekeza katika sekta hizo ili kuimarisha nguvu kazi, kuongeza utaalamu na kuboresha utoaji wa huduma, hususan katika sekta ya utalii na maendeleo ya uchumi wa buluu.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha sera bora za uwekezaji pamoja na kuendeleza miundombinu ya barabara na bandari, ikiwemo Bandari Jumuishi ya Mangapwani, ambayo itakapokamilika itatoa fursa pana za uwekezaji.

Amesisitiza kuhusu mkakati wa kukifungua Kisiwa cha Pemba kuwa kituo cha uwekezaji na utalii endelevu.
Rais Dkt.Mwinyi ameihakikishia Ufaransa kuwa Zanzibar itaendelea kuendeleza mikakati ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi, na amewasisitiza wawekezaji kutoka Ufaransa kuja Zanzibar kujionea na kubaini fursa zilizopo.
Naye Balozi Anne Sophie ameihakikishia Zanzibar kuwa Ufaransa itaendelea kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa katika kuimarisha maeneo muhimu ya kiuchumi, hususan miradi ya sekta za utalii, afya, elimu, utamaduni, uendelezaji wa Mji Mkongwe, mazingira na uchumi wa buluu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here