ACP Ngiichi akutana na waendesha bodaboda

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Gerald Ngiichi amefanya ziara maalum katika barabara kuu inayounganisha mikoa ya kusini mwa Tanzania, ambako alipata fursa ya kukutana na waendesha bodaboda wanaofanya shughuli zao katika vijiwe mbalimbali vilivyopo pembezoni mwa barabara hiyo.
Katika ziara hiyo, Kamishna Msaidizi Ngiichi alizungumza na madereva hao na kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati pindi wanapobaini au kuhisi kuwepo kwa viashiria vya uhalifu katika maeneo yao.

Akizungumza na kundi hilo, Ngiichi alieleza kuwa waendesha bodaboda ni sehemu muhimu ya jamii kwa kuwa mara nyingi wao ndio wanaokuwa wa kwanza kuona au kukutana na matukio mbalimbali yanayotokea barabarani na katika maeneo ya jirani.

Alisisitiza kuwa, taarifa wanazoweza kuzitoa zina mchango mkubwa katika kuzuia, kudhibiti na hata kufichua vitendo vya uhalifu.
Aidha, aliwakumbusha umuhimu wa kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, hususan zile zinazohusu usalama barabarani.

Miongoni mwa mambo aliyoyasisitiza ni pamoja na matumizi ya kofia ngumu (helmet), kubeba abiria kwa usalama, pamoja na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao na ya abiria wanaowahudumia.

Kwa upande wao, baadhi ya waendesha bodaboda waliopata fursa ya kuzungumza walimshukuru Kamishna Msaidizi huyo kwa kuwafikia moja kwa moja katika maeneo yao ya kazi.

Walieleza kuwa, hatua hiyo imewapa motisha ya kuimarisha ushirikiano wao na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kudumisha amani, utulivu na usalama katika Mkoa wa Lindi na maeneo ya jirani.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada zinazoendelea za Jeshi la Polisi za kuimarisha ushirikiano na jamii, sambamba na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu wajibu wao katika kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here