NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 329 wanaodaiwa kuhusika na makosa mbalimbali ya jinai katika operesheni, misako na doria zilizofanyika katika maeneo tofauti ya mkoa huo kuanzia Machi 1 hadi Machi 8, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga imeeleza kuwa, watuhumiwa hao wanakabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo mauaji, kupatikana na silaha bila kibali, kupatikana na nyara za serikali zikiwemo meno ya tembo, kupatikana na pombe haramu pamoja na dawa za kulevya.Katika operesheni hizo, Polisi wanawashikilia Ostin Angolile Mwangulukuru (40), mkazi wa Ndwanga, pamoja na Frank Adamson Mwakiluma (46), mkazi wa Ngonga, kwa tuhuma za kupatikana na vipande tisa vya meno ya tembo.
Watuhumiwa hao walikamatwa Machi 5, 2026 majira ya saa 9:30 alfajiri katika nyumba ya kulala wageni iliyopo kitongoji cha Jonard, Kata ya Mikoroshini, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela.
Wakati wa kukamatwa kwao walikutwa wakiwa wamehifadhi vipande hivyo vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 30 ndani ya mfuko wa sandarusi wakitafuta wateja.
Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa tukio hilo lilichochewa na tamaa ya kujipatia fedha kwa njia zisizo halali.
Katika tukio lingine, Polisi walifanikiwa kukamata bunduki moja aina ya RK62 iliyokuwa imefutwa namba zake pamoja na risasi mbili zenye kaliba ya 7.62mm katika eneo la pori la hifadhi ya Lukwati lililopo katika Kijiji na Kata ya Kambikatoto.
Tukio hilo lilitokea Machi 5, 2026 majira ya saa 8:30 mchana, ambapo mtuhumiwa aliyetambulika kwa jina la Sukari George alifanikiwa kutoroka na kuiacha silaha hiyo.
Polisi wamesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mtuhumiwa huyo ni muwindaji haramu na juhudi za kumsaka zinaendelea.
Aidha, katika operesheni nyingine ya misako, Polisi wanamshikilia Mwinyi Juma Shupika (36), mkazi wa Soweto “B”, kwa tuhuma za kupatikana na bunduki aina ya Shotgun bila kibali.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 5, 2026 majira ya saa 8:30 usiku katika Kitongoji cha Soweto, Kata ya Kasanga, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya akiwa na silaha hiyo iliyokuwa imetunzwa ndani ya mfuko pamoja na risasi nane za Shotgun zenye kaliba ya 12mm.
Katika upekuzi uliofanywa nyumbani kwa mtuhumiwa huyo, Polisi walikuta panga, kisu na tochi, vifaa vinavyoashiria kuwa alijihusisha na vitendo vya uwindaji haramu.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi linawashikilia Baraka George Daniel (24) na Mussa Israel Mwakyembe (27), wote mafundi umeme na wakazi wa Bulyaga, Wilaya ya Rungwe, kwa tuhuma za kuingilia miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Watuhumiwa hao walikamatwa Machi 7, 2026 katika Kijiji cha Isebe, Kata ya Itagata, Tarafa ya Pakati, Wilaya ya Rungwe, wakidaiwa kufungua nyaya za umeme za shaba (copper) kutoka kwenye nguzo za umeme za shirika hilo zilizopo katika barabara ya Katumba–Mwakareli bila kibali.
Polisi wamesema nyaya hizo ni muhimu kwa mfumo wa usambazaji wa umeme na kuondolewa kwake kunaweza kuathiri huduma ya umeme katika maeneo husika.
Upelelezi zaidi unaendelea ili kubaini mtandao wa wahusika wengine wanaodaiwa kushiriki katika vitendo hivyo.
Katika operesheni hizo pia Polisi walikamata mtuhumiwa mmoja akiwa na pombe haramu ya moshi maarufu kama gongo yenye ujazo wa lita 24.5, watuhumiwa wawili waliokutwa na dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 25, pamoja na watuhumiwa wengine katika matukio tofauti ya mauaji, wizi wa simu na matukio 16 ya uporaji, uvunjaji na wizi katika nyumba za makazi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kulinda rasilimali za taifa pamoja na kudumisha amani na usalama.
Aidha, limewataka wale wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja, likisisitiza kuwa uhalifu haulipi na hautavumiliwa katika jamii.
