MANYARA-Katika Mahakama ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Machi 25,2026 limefunguliwa shauri la uhujumu uchumi namba 6525/2026 linalomkabili aliyekuwa Afisa Ardhi mteule wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Bw. Samwel Donald Lyimo.
Shauri hilo linasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mheshimiwa Jumaa Mwambago, ambapo mshtakiwa anakabiliwa na tuhuma za kushindwa kukidhi matakwa ya kisheria ya kuwasilisha tamko sahihi la mali anazomiliki.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Bw. Lyimo anadaiwa kutoa taarifa za uongo kuhusu viwanja anavyomiliki, kinyume na kifungu cha 26(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya mwaka 2023. Kifungu hicho kinasomwa pamoja na aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 61(2) vya Sheria ya Kudhibiti Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa, Sura ya 200, Marejeo ya mwaka 2023.
Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo, Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi. Neema Gembe, alidai kuwa mshtakiwa, akiwa mtumishi wa umma katika nafasi ya Afisa Ardhi mteule, alikiuka matakwa ya kisheria kwa kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu mali zake, hususan viwanja.
Mshtakiwa alikana shtaka hilo aliposomwa mashtaka yake mahakamani hapo.
Hata hivyo, alishindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama, hali iliyosababisha kupelekwa rumande hadi atakapokidhi vigezo hivyo.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Machi 26, 2026, ambapo mahakama inatarajiwa kusikiliza maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na upande wa utetezi.
