Barabara ya kisasa Kibaha hadi Chalinze mbioni

NA DIRAMAKINI

SERIKALI imeanza upya mchakato wa utekelezaji wa mradi wa barabara ya kisasa ya Kibaha–Chalinze, baada ya kufanya maboresho katika mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), hatua inayolenga kuondoa vikwazo vilivyochelewesha mradi huo kwa muda mrefu.
Akizungumza katika mjadala wa kitaifa kuhusu ubia huo uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha PPP, David Kafulila alisema, Serikali imefanya marekebisho muhimu ya kimkakati ili kufufua mradi huo na kuvutia wawekezaji wapya.

Kwa mujibu wa Kafulila, marekebisho hayo yanalenga kuboresha mchakato wa manunuzi, kuongeza uwazi na kuimarisha mazingira ya uwekezaji ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi.

Barabara ya Kibaha–Chalinze yenye urefu wa takribani kilometa 78.9 ni sehemu muhimu ya ukanda wa usafiri unaounganisha Dar es Salaam na mikoa ya ndani ya nchi pamoja na nchi jirani zisizo na bandari.

Aidha, ni miongoni mwa barabara zenye msongamano mkubwa wa magari nchini kutokana na kupitisha magari ya abiria na mizigo kuelekea mikoa ya Morogoro, Dodoma na kanda ya kati pamoja na nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Serikali inaamini kuwa, kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kupunguza msongamano wa magari, kuharakisha usafirishaji wa mizigo na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayohudumiwa na barabara hiyo.

Mradi huo ulianza maandalizi yake mwaka 2017 kwa lengo la kujengwa kwa mfumo wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi, lakini ulikumbwa na changamoto mbalimbali katika hatua za manunuzi na majadiliano na wawekezaji.

Katika hatua za mwisho za mchakato huo, mzabuni mmoja pekee alibaki kwenye majadiliano baada ya kampuni nyingine kujiondoa. Hata hivyo, makadirio ya gharama yaliyowasilishwa na mzabuni huyo yalikuwa makubwa zaidi kuliko makadirio ya serikali.

Inadaiwa kuwa, mzabuni alipendekeza gharama za zaidi ya dola milioni 900, wakati serikali ilikuwa imekadiria gharama za mradi huo kuwa takribani dola milioni 560, hali iliyosababisha majadiliano kusimama.
Mpango mpya wa utekelezaji

Kutokana na hali hiyo, serikali imeanza kuandaa mfumo mpya wa utekelezaji ili kuhakikisha mradi huo unapata wawekezaji wengi zaidi na kufanikisha utekelezaji wake kwa wakati.

Matarajio ya Wananchi

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wanaotumia barabara hiyo mara kwa mara, mkazi wa Chalinze, Mwinjilisti wa Kimataifa, Dkt.Alphonce Temba amesema kuwa, kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kupunguza msongamano wa magari na ajali ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara katika barabara hiyo.

Dkt.Temba amesema kuwa, kwa sasa barabara hiyo inabeba idadi kubwa ya magari ya mizigo na abiria yanayoelekea mikoa ya ndani ya nchi pamoja na nchi jirani, hali inayosababisha msongamano mkubwa hasa nyakati za asubuhi na jioni.

“Tunaomba Serikali iharakishe utekelezaji wa mradi huu kwa sababu barabara ya Kibaha-Chalinze ni muhimu sana kwa uchumi na usafiri wa wananchi. Kukamilika kwake kutarahisisha safari na kupunguza foleni ambazo zimekuwa zikisumbua watumiaji wa barabara hii kwa muda mrefu.”

Pia amependekeza kuwa, katika utekelezaji wa mradi huo, Serikali izingatie viwango vya ubora wa ujenzi pamoja na kuweka miundombinu ya kisasa ya usalama barabarani ili kulinda maisha ya watumiaji wa barabara.

Naye dereva wa lori la mizigo, Said Khamis amesema, barabara hiyo ni muhimu kwa usafirishaji wa mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya ndani ya nchi pamoja na nchi jirani.

“Barabara hii ndiyo njia kuu ya magari mengi ya mizigo. Mara nyingi tunakaa kwenye foleni kwa muda mrefu hasa Kibaha na Chalinze. Kama barabara ya kisasa itajengwa, safari zitakuwa fupi na gharama za usafirishaji zitapungua."

Mfanyabiashara wa bidhaa za chakula katika eneo la Chalinze, Aisha Mohamed amesema mradi, huo utaongeza fursa za biashara kwa wakazi wa maeneo ya jirani.

“Kupita kwa magari mengi kunaleta wateja na kukuza biashara. Tukipata barabara ya kisasa, shughuli za kiuchumi katika maeneo haya zitaongezeka zaidi."

Julius Amon ambaye ni mtumiaji wa barabara hii kwa safari za mara kwa mara mikoani anasema, "ujenzi wa kisasa ni muhimu, kwani barabar hii inatumiwa na watu wengi sana wanaosafiri kwenda mikoa ya kati na kaskazini. Kukamilika kwake kutapunguza foleni na kufanya safari kuwa salama na rahisi zaidi,"amesema.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya miundombinu, kukamilika kwa barabara ya kisasa ya Kibaha-Chalinze kutakuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya ndani ya nchi na mataifa jirani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here