Benki Kuu yauza Dola milioni 20 katika Soko la Fedha za Kigeni

NA DIRAMAKINI

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeuza dola za Marekani milioni 20 katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni (IFEM) kupitia mnada wa ushindani.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera yake ya mwaka 2023 inayoruhusu ushiriki wa benki hiyo katika soko hilo kwa lengo la kuimarisha ukwasi wa fedha za kigeni nchini.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 16,2026 na Kurugenzi ya Masoko ya Fedha (Directorate of Financial Markets) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mnada huo umefanyika kwa kiwango cha wastani cha ubadilishaji wa Shilingi 2,592.85 kwa dola moja ya Marekani.

Aidha,hatua hiyo inalenga kusaidia kudhibiti mwenendo wa soko na kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kigeni kwa taasisi za kifedha nchini.

Katika mnada huo, kiasi kilichotangazwa kwa ajili ya kuuzwa kilikuwa dola milioni 20, huku maombi yaliyowasilishwa na benki mbalimbali yakifikia dola milioni 25.5. Hata hivyo, kiasi kilichokubaliwa kuuzwa kilibaki dola milioni 20 kama kilivyopangwa.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, kiwango cha juu cha ushindani katika mnada kilifikia Shilingi 2,596 kwa dola moja, wakati kiwango cha chini kilikuwa Shilingi 2,580 kwa dola moja.

Kwa upande wa viwango vilivyokubaliwa, kiwango cha juu kilikuwa Shilingi 2,596 kwa dola moja na kiwango cha chini kilikuwa Shilingi 2,590 kwa dola moja.

Aidha, jumla ya benki 20 zilishiriki katika mnada huo, ambapo benki 15 zilifanikiwa kushinda zabuni na kupata mgao wa fedha za kigeni.

Ushiriki wa BoT katika soko la fedha za kigeni ni sehemu ya mikakati ya kusimamia utulivu wa masoko ya fedha na kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kigeni kwa mahitaji ya uchumi wa nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here