TANGA-Mbunge wa Jimbo la Lushoto,Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ametoa msaada wa chakula cha futari jimboni kwake kwa wanafunzi wa shule za Sekondari kidato cha Tano na Sita za Shambalai, Magamba, Mlongwema, Ubiri na Masange juu.
Msaada huo wa chakula hicho cha futari umetolewa kwa niaba yake na waheshimiwa madiwani kwa wanafunzi wa shule hizo jana Machi 15, 2026 katika kata ambazo shule hizo zipo, huku wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Lushoto.
Miongoni mwa vyakula vilivyotolewa kwa wanafunzi wa shule hizo ni pamoja na unga wa ngano, unga wa sembe, mchele, ndizi, mafuta, mihogo na viazi.
Kwa upande wao, wanafunzi wa shule hizo wamemshukuru Prof. Shemdoe kwa kuwapatia msaada wa vyakula hivyo ambavyo vitawawezesha kuwapa nguvu ya kuendelea na masomo wakiwa katika ibada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na Kwaresma.Aidha, Waheshimiwa Madiwani hao kwa niaba ya Prof. Shemdoe wamekabidhi Shilingi 200,000 kwenye Kituo cha Watoto yatima Irente kwa ajili ya kuwawezesha watoto wa kituo hicho kupata zawadi ya Sikukuu ya Idd.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto Prof. Shemdoe ameendelea kutoa msaada wa chakula cha futari kwa makundi yenye uhitaji jimboni kwake, kwani siku mbili zilizopita alishirikiana na Taasisi ya Islamic Help kutoa msaada wa chakula cha futari kwa kaya 100 za Ubiri na Ngulwi jimboni humo.