DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amefanya kikao na ujumbe kutoka Shirika la Uwekezaji la China (China Investment Corporation-CIC) ulioongozwa na Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Vihatarishi na Makamu wa Rais Mtendaji, Bw. Guo Xiangjun. Kikao hicho kimefanyika kwa njia ya mtandao tarehe 24 Machi 2026.
Katika kikao hicho, Gavana Tutuba alieleza kuwa, Serikali ya Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuweka sera na mifumo rafiki pamoja na kupunguza urasimu, hatua inayolenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, alibainisha kuwa kwa sasa Serikali inatekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifikisha Tanzania katika hadhi ya nchi yenye uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu. Katika utekelezaji wa dira hiyo, matarajio ni kuwa ifikapo mwaka 2050, pato la taifa litafikia thamani ya dola za Marekani trilioni moja, huku wastani wa pato la mtu mmoja ukifikia dola za Marekani 7,000 kwa mwaka.
Katika kufanikisha azma hiyo, Gavana Tutuba alitaja sekta mbalimbali zenye fursa kubwa za uwekezaji, ikiwemo kilimo, utalii, viwanda na uzalishaji, madini, uchumi wa buluu, michezo na ubunifu, sekta ya fedha pamoja na sekta ya huduma.
Mwisho wa kikao hicho, pande zote mbili ziliazimia kuendeleza na kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya uwekezaji, kubadilishana uzoefu pamoja na kujenga uwezo, kwa lengo la kukuza maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla.

