NA DIRAMAKINI
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeuza jumla ya Dola za Marekani milioni 20 katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni (Interbank Foreign Exchange Market-IFEM) kupitia mnada wa ushindani, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuongeza ukwasi na kuimarisha utulivu katika soko la fedha za kigeni nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na BoT, hatua hiyo imefanyika kwa kuzingatia Sera ya Ushiriki katika Soko la Fedha za Kigeni ya mwaka 2023.
Aidha, katika mnada huo, dola hizo ziliuzwa kwa kiwango cha wastani cha ubadilishaji wa Shilingi 2,575.22 kwa dola moja ya Marekani.
Lengo kuu la mnada huo lilikuwa kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni katika soko la ndani na kusaidia kuimarisha mwenendo wa biashara za fedha za kigeni kati ya benki.
Katika mnada huo, kiasi kilichotangazwa kwa ajili ya kuuzwa kilikuwa Dola milioni 20, huku zabuni zilizowasilishwa na benki mbalimbali zikifikia Dola milioni 21.25. Hata hivyo, kiasi kilichokubaliwa kilibaki kuwa Dola milioni 20 kama kilivyopangwa.
Taarifa hiyo inaonesha kuwa,kiwango cha juu cha zabuni kilikuwa Shilingi 2,586 kwa dola moja, wakati kiwango cha chini kilikuwa Shilingi 2,560 kwa dola moja. Viwango hivyo hivyo ndivyo vilivyokubalika katika zabuni zilizofanikiwa.
Jumla ya benki 13 zilishiriki katika mnada huo, na zote zilifanikiwa kukubaliwa katika mchakato wa ugawaji wa fedha hizo.

