BoT yasisitiza nafasi ya wanawake katika Mfumo Jumuishi wa Fedha

ARUSHA-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anayesimamia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, amesisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za uongozi ili kufanikisha malengo ya ujumuishwaji wa kifedha nchini.
Bi. Msemo amesema hayo katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWIFA), wenye kaulimbiu “Uongozi wa Wanawake kama Kichocheo cha Mifumo Jumuishi na Endelevu ya Kifedha: Kuendeleza NFIF III na FSDMP 2030” uliofanyika tarehe 23 Machi 2026 jijini Arusha.

Alieleza kuwa kufikiwa kwa malengo ya Mkakati wa Kitaifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (NFIF III) na Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (FSDMP) kunahitaji jitihada za makusudi za kuziba pengo la kijinsia.

Alisisitiza kuwa wanawake hawapaswi kuonekana tu kama wanufaika wa huduma za kifedha, bali washirikishwe kikamilifu kama wabunifu na wachangiaji wa mifumo bora ya kifedha.

Alibainisha kuwa wanawake wengi wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa dhamana zinazokubalika na taasisi za fedha, kutokana na wengi wao kutomiliki mali zisizohamishika kama ardhi.

Kutokana na hali hiyo, Benki Kuu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha inaandaa rasimu ya sheria itakayoruhusu matumizi ya mali zinazohamishika ikiwemo vifaa, mazao, hisa na mali nyingine kama dhamana ya mikopo
Aidha, Naibu Gavana alibainisha vikwazo vya kimasoko, ikiwemo uwepo wa bidhaa za kifedha zisizoendana na mahitaji ya wanawake, gharama kubwa za miamala na upatikanaji mdogo wa huduma katika maeneo ya vijijini.

Alitoa wito kwa taasisi za fedha na kampuni za teknolojia ya fedha (Fintech) kuendelea kubuni bidhaa jumuishi zinazolenga kuwafikia wanawake, hususan waliopo katika sekta isiyo rasmi.

Kwa upande wa vikwazo vya watumiaji wa huduma, alitaja changamoto za uelewa mdogo wa masuala ya kifedha, mila na desturi, pamoja na uaminifu mdogo kwa taasisi rasmi za kifedha.
Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu ya fedha na programu za kujenga uwezo, pamoja na kutumia mifumo ya kijamii kama vikundi vya kuweka akiba ili kuongeza ushiriki wa wanawake.

Mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here