DAR-Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo (Mb), amesema Tanzania iko tayari kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Austria unaolenga kukuza sekta za viwanda na biashara kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mheshimiwa Londo ameyasema hayo leo Machi 23, 2026 jijini Dar es Salaam alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria, Mhe. Balozi Dkt. Hannah Liko aliyepo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, ambapo amesisitiza kuwa ziara hiyo ni daraja muhimu la kufungua milango ya fursa za kiuchumi kati ya Tanzania na Austria.
Amebainisha kuwa, Tanzania imejipanga kwa kuweka mazingira rafiki na salama kwa wawekezaji wa kimataifa, huku akiwakaribisha wawekezaji kutoka Austria kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, kilimo, biashara na madini ili kuchochea ukuaji wa uchumi.Aidha, Mhe. Londo amesema kutokana na kasi ya mapinduzi ya viwanda duniani, kuna uhitaji mkubwa wa wataalamu, hivyo ni muhimu kwa pande hizo mbili kuendelea kubadilishana uzoefu, teknolojia na ujuzi wa kitaalamu ili kuleta manufaa ya pamoja.
Kwa upande wake, Dkt.Liko amesema Austria imedhamiria kuendelea kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, ajira na utalii.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara.
Ameongeza kuwa Austria itaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa Watanzania pamoja na kuendeleza ushirikiano na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), hatua ambazo ni sehemu ya Mkakati wa Afrika wa Austria (2026–2029) unaolenga kuimarisha utawala bora, haki za binadamu na maendeleo endelevu kupitia sekta za umma na binafsi.





