NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo mpya za bidhaa za mafuta ya petroli zitakazoanza kutumika rasmi kuanzia saa 6:01 usiku wa kuamkia Machi 4,2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei hizo zinahusu petroli, dizeli na mafuta ya taa zilizoingizwa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, ambapo viwango vya rejareja na jumla vimeainishwa kulingana na gharama halisi za uagizaji na mwenendo wa soko la dunia.
Katika Mkoa wa Dar es Salaam bei za rejareja, petroli itauzwa kwa Sh 2,864 kwa lita, dizeli Sh 2,858 na mafuta ya taa Sh 2,932.
Tanga, petroli itakuwa Sh 2,925, dizeli Sh 2,919 na mafuta ya taa Sh 2,993 kwa lita na Mtwara, petroli itauzwa kwa Sh 2,956, dizeli Sh 2,951 huku mafuta ya taa yakifikia Sh 3,025 kwa lita.
Kwa upande wa bei za jumla, Dar es Salaam petroli ni Sh 2,723.97, dizeli Sh 2,718.21 na mafuta ya taa Sh 2,792.70.Tanga, petroli ni Sh 2,721.05 na dizeli Sh 2,719.86 huku Mtwara, petroli ni Sh 2,727.04 na dizeli Sh 2,730.20.
EWURA imeeleza kuwa, bei za mafuta hapa nchini zinategemea gharama za mafuta yaliyochakatwa katika soko la dunia (FOB) pamoja na gharama za uagizaji katika soko la Afrika Mashariki.
Katika mwezi Machi 2026, bei za mafuta katika soko la dunia zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 6.2 kwa petroli, asilimia 9.8 kwa dizeli na asilimia 7.4 kwa mafuta ya taa.
Aidha, gharama za uagizaji (premiums) katika Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka kwa asilimia 0.07 kwa petroli na asilimia 10.76 kwa dizeli, huku gharama za mafuta ya taa zikishuka kwa asilimia 5.41. Hakukuwa na mabadiliko ya gharama za uagizaji katika bandari za Tanga na Mtwara.
Vilevile, wastani wa viwango vya kubadilisha fedha za kigeni (Applicable Exchange Rate) umeongezeka kwa asilimia 8.54, hali iliyochangia kupanda kwa gharama za mafuta.
Maagizo kwa Wafanyabiashara
EWURA imewataka wafanyabiashara wa rejareja na jumla kuzingatia bei zilizoainishwa, ikisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka agizo hilo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta zinaendelea kupangwa kwa kuzingatia misingi ya soko huria lenye ushindani.
Hata hivyo, kampuni haziruhusiwi kuuza juu ya bei kikomo (Price Cap) au chini ya bei iliyoruhusiwa (Floor Price) kama ilivyobainishwa katika kanuni husika.
Vituo vyote vya mafuta vimetakiwa kuonesha bayana mabango ya bei yanayoonekana kwa urahisi kwa wateja. Pia, wauzaji wanapaswa kutoa stakabadhi za mauzo kupitia mashine za Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP) zikionesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta na bei kwa lita.
Licha ya changamoto zinazoendelea katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati, EWURA imesisitiza kuwa nchi ina mafuta ya kutosha kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea bila kukwama.

.jpeg)

