DCEA yakamata tani 9.93 za dawa za kulevya,watuhumiwa 151 wadakwa

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata tani 9.93 za dawa za kulevya aina mbalimbali ikiwemo chupa 1,795 za dawa tiba zenye asili ya kulevya na kutekeleza ekari 87.5 za mashamba ya bangi.
Hayo yamesemwa leo Machi 4,2026 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, ukamataji huo umetokana na operesheni kabambe iliyoendeshwa na mamlaka hiyo kote nchini katika kipindi cha mwezi Januari na Februari,2026.

Amesema kuwa,pia magari sita na pikipiki 29 wakiwemo watuhumiwa 151 walikamatwa katika operesheni hizo.

Kamishna Kamishna Jenerali Lyimo ameongeza kuwa, pia kwa kushirikiana na maafisa wa kituo cha forodha cha Mutukula, mamlaka imekamata dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Pethidine boksi 105 zenye chupa 1,045, Morphine Sulphate boksi 31 zenye chupa 310 na Fentanyl boksi 44 zenye chupa 440.
Amesema,dawa hizo zilikamatwa katika basi la abiria la kampuni ya SR Classic lenye usajili wa nchi ya Congo namba 5673AB04, linalofanya safari zake kati ya nchi za Uganda, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

"Dawa zilizokamatwa zilibainika wakati wa upekuzi wa basi hilo katika kituo cha forodha cha Mutukula lilipokuwa likiingia nchini Tanzania.

Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo, Kamishna Jenerali Lyimo amewataja ni Hassan Omary Mwambashi maarufu kama Macheni (50) mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, Ibrahim Saidi Malindi (36), mtanzania anayeishi Kampala Uganda na Yassa Said Hamood (38) mkazi wa Magomeni Dar es Salaam.

Wengine ni Hamad Said Hamad (46) mkazi wa Mombo Tanga, Abdul Athuman Khamis (31) mkazi wa Amana, Dar es Salaam, Mohamed Abdallah Sako (34) mkazi wa Ilala na Mwinshaa Mohamed Abdalla (47) mkazi wa Magomeni Dar es Salaam.
Amesema,dawa aina ya Pethidine, Morphine na Fentanyl ni dawa tiba zenye asili ya kulevya zilizopo kwenye kundi la afyuni (opioids) ambazo hutumika hospitalini kwa ajili ya kupunguza maumivu makali wakati wa operesheni, kwa wagonjwa wa saratani, ajali, pamoja na wagonjwa wa selimundu.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, dawa hizi zikichepushwa zinaweza kutumika kama dawa za kulevya na kusababisha uraibu kwa haraka zaidi kutokana na kuwa na nguvu kubwa.

"Dawa hizi zipo katika kundi la vipumbazi na zina uwezo mkubwa wa kusababisha vifo kwa haraka kwa mtumiaji, kwani huharibu mifumo ya mwili hasa mapigo ya moyo, mfumo wa fahamu na mfumo wa upumuaji."

Amesema,hapa nchini, dawa zilizokamatwa zinadhibitiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95 na Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba ya TMDA Sura ya 219.

Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imeorodhesha dawa hizo katika Jedwali la Kwanza (First Schedule) na Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba inabainisha kuwa, muingizaji na msambazaji wa dawa aina ya nakotiki ni Medical Store Department (MSD) pekee.
Kwa upande wa dawa za kulevya, bangi aina ya skanka imeendelea kukamatwa kwa wingi nchini. Katika operesheni zilizofanyika jijini Dar es Salaam, mtuhumiwa Jontwa Samwel Mwaikonyole (43) mkazi wa Gogoni Kibamba, alikamatwa akiwa na kilogramu 81.883 za skanka zikiwa ndani ya gari aina ya Scania lenye namba za usajili wa nchi ya Afrika ya Kusini CAA 129054 na trailer namba CAA 22911 lililokuwa limebeba matunda aina ya apples.

Pia, amesema eneo la Chanika Buyuni watuhumiwa Masudi Rajabu (38) na mwenzake Shafii Mohamed (30) walikamatwa wakiwa na kilogramu 488.64 za skanka.

Aidha, katika ukaguzi wa mabasi ya abiria jijini Mbeya, watuhumiwa sita walikamatwa kwa nyakati tofauti wakisafirisha bangi aina ya skanka.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, watuhumiwa hao ni Lenard Paulo (21) mkazi wa Sirali Mara ambaye alikamatwa na kilogramu 46.46 , Maria Kandonga (18) na wenzake Monica Kandonga (41) na Ibrahim Mwakibete (26) wote wakazi wa Mbeya, walikamatwa wakiwa na kilogramu 9.68.
Kwa upande wa mtuhumiwa Joseph Mkwala (30) raia wa Malawi alikamatwa na kilogramu 4.62 na Esther Mbise (22) mkazi wa Mbeya alikamatwa na kilogramu 16.1 za skanka.

Aidha,mkoani Arusha, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, watuhumiwa Fatuma Mussa Mohamed (45) maarufu kwa jina la Mama Arapha na mwenzake Elibaraka Martin Kingu (29) maarufu kwa jina Baraka walikamatwa wakiwa na bunda 937 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 363.45.

"Mama Arapha ni mhalifu wa muda mrefu aliyekuwa akiendesha mitandao ya usafirishaji wa mirungi. Vilevile, katika operesheni zilizofanyika mikoa ya Tabora, Tanga, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Katavi, Mtwara, Mara, Morogoro, Kigoma, Ruvuma na Kilimanjaro zilikamatwa tani 5.24 za dawa za kulevya aina ya bangi, tani 4.04 za mirungi pamoja na gramu 72 za heroin,"ameongeza Kamishna Jenerali Lyimo.

Amesema, operesheni zilizofanyika zinaonesha jitihada za Serikali katika kupunguza upatikanaji wa dawa za kulevya nchini.

"Mamlaka itaendelea kupambana na wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya pamoja na dawa tiba zenye asili ya kulevya ili kuhakikisha hazichepushwi na zinawafikia wagonjwa wanaohitaji dawa hizo badala ya kutumiwa na wahalifu kama mbadala wa dawa za kulevya.
"Mamlaka itaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za Serikali, Mashirika, Asasi za kiraia pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii kuhakikisha kwamba, tatizo la dawa za kulevya linadhibitiwa kikamilifu kwani mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja wetu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here