Gavana Tutuba ashiriki maziko ya Gavana mstaafu Dkt.Idris Rashid mkoani Manyara

MANYARA-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba ameshiriki katika shughuli za maziko ya Gavana mstaafu wa Benki Kuu, Hayati Dkt. Idris M. Rashid, yaliyofanyika Machi 14,2026 katika Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara.
Akizungumza na waombolezaji waliohudhuria maziko hayo, Gavana Tutuba alisema kuwa,Dkt.Rashid ameacha alama muhimu katika mageuzi ya kiuchumi nchini wakati wa uongozi wake kama Gavana kuanzia mwaka 1993 hadi 1998.

Alieleza kuwa,miongoni mwa mafanikio makubwa ya uongozi wake ni kusimamia mabadiliko ya Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 1995.

Kutokana na hatua hiyo, alisema Dkt. Rashid alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha misingi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia mageuzi na dira aliyoiweka wakati wa utumishi wake.
Aidha, Gavana Tutuba aliwahimiza wananchi kumuenzi Dkt.Rashid kwa kuendeleza misingi ya uzalendo, uadilifu na bidii katika kazi, kama alivyoonyesha wakati wa utumishi wake, kwa lengo la kuchangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja, jamii na Taifa kwa ujumla.

Kwa kuhitimisha, Gavana Tutuba alieleza kuwa Hayati Dkt.Rashid alikuwa mtu mcha Mungu, mwenye upendo kwa watu wote na mwenye moyo wa kusaidia wengine.
Kutokana na sifa hizo njema, aliwataka wananchi kumuenzi kwa kuiga mienendo yake ya kushika na kuheshimu dini, kuwajali na kuwasaidia wengine, kuishi kwa upendo pamoja na kudumisha mshikamano na maelewano katika jamii.
Maziko hayo pia yalihudhuriwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Ali Munde (Mb), pamoja na wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania, walioungana na familia, ndugu na marafiki katika kutoa heshima za mwisho kwa Hayati Dkt. Idris M. Rashid.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here