Hakuna shirika la Umoja wa Mataifa lililojiondoa kuisaidia Tanzania-Balozi Possi

NA GODFREY NNKO

MWAKILISHI wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Dkt. Abdallah Possi amewatoa hofu Watanzania kufuatia madai yanayosambaa mitandaoni kwamba, baadhi ya mashirika ya kimataifa yamejiondoa katika kuunga mkono miradi ya maendeleo nchini.
Ameyasema hayo leo Machi 4,2026 alipofanya mkutano wake na waandishi wa habari mbalimbali nchini akiwa mjini Geneva, Uswisi kwa njia ya mtandao.

Balozi Possi ambaye anahudhuria kikao cha 61 cha Baraza la Haki za Binadamu Umoja wa Mataifa (UNHRC), kinachofanyika mjini Geneva amesema,hakuna shirika, hususan yale yaliyo chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa, lililochukua uamuzi wa kusitisha au kujiondoa katika kutoa misaada kwa Tanzania kutokana na matukio ya Oktoba 29, 2025.

Amefafanua kuwa, hali inayoonekana sasa siyo ya kujiondoa kwa makusudi, bali ni changamoto ya kifedha inayozikabili taasisi nyingi za kimataifa, kufuatia mabadiliko ya sera za ufadhili katika baadhi ya nchi wafadhili wakuu.

Balozi Possi ameeleza kuwa, baadhi ya mashirika yamelazimika kuelekeza rasilimali chache zilizopo katika maeneo yenye migogoro na vita, ambako mahitaji ya kibinadamu ni makubwa zaidi.

"To be honest, kwa sasa hakuna shirika la Umoja wa Mataifa lililojiondoa kuisaidia Tanzania. Kilichopo ni changamoto ya jumla ya upungufu wa fedha katika mfumo wa kimataifa wa misaada, kama kuna hiyo kauli haijawahi kutokea hapa Geneva, kwa sababu hapa Geneva tuna deal na World Trade Organization, WHO, UNHRC, na kadhalika.

"Kitu ambacho ninaweza nikasema ni kwamba, hapa Geneva mashirika mengi yamekumbwa na ukata wa fedha kutokana na Marekani kujitoa katika baadhi ya mashirika na baadhi ya nchi kupunguza michango yake."

Amesema, kwa sasa nchi nyingi zinashirikiana kwa karibu na Ukraine katika masuala ya ulinzi.Hivyo progamu nyingi za mashirika ya Umoja wa Mataifa zimeathiriwa kutokana na ukata ikiwemo ufinyu wa bajeti.

Katika hatua nyingine, Balozi Dkt. Abdallah Possi amewahimiza Watanzania bila kujali rika, kabila, wasifu au itikadi kuendelea kudumisha amani ya nchi ili Taifa liweze kusonga mbele ikizingatiwa kwamba, Dunia kwa sasa inapitia kipindi kigumu katika nyanja mbalimbali hivyo unachopoteza sasa ni vigumu kukirejesha kwa muda mfupi.

Katika hatua nyingine, Balozi Possi amesema kuwa, kutokana na mabadiliko ya kisera na hali ya kisiasa ya Dunia, mataifa mengi yameanza kujiondoa katika utaratibu wa kutoa misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo na sasa wapo kibiashara zaidi.

"Kwa hiyo, maana yake ni nini? Kiukweli kabisa sidhani kuwa kama itakuwa sahihi kwa Watanzania kudhani miaka 30 au miaka 20 ijayo sisi tuendelee tu kupewa misaada, kuna msaada ambao hauna masharti ni namna gani unaweza kufaidika, inategemea sasa na wewe ni namna gani utautweza utu wako.

"Na ukumbuke hiyo hela inayotolewa na wenzetu ni ya walipa kodi wao, na mabadiliko ya kisiasa kwenye nchi nyingi za Ulaya ambazo zinaingia katika siasa za mrengo wa kulia, wapo kujiangalia wao.

"Kwa hiyo, kwa hali hiyo lazima tujue kupunguza misaada au kuondoa kabisa ni suala tu la muda, kwa hiyo nchi zetu za Afrika ikiwemo Tanzania itabidi tusimame wenyewe."

Kwa muktadha huo, Dkt.Possi anasisitiza kuwa, njia nzuri zaidi ni kwa nchi zetu kuangalia namna bora ya kujiandaa mapema ili kuweza kusimama zenyewe bila utegemezi wa kiuchumi kutoka nje.

Amesema, miongoni mwa viashiria vya misaada hiyo kuanza kuwa na masharti magumu kwa nchi tegemezi ni pamoja na kuhimizwa kutekeleza mambo ambayo yapo kinyume na maadili huku kwa yale yenye uchumi imara hawawezi kunyoosha kidole kwao.

"Na Mwafrika yeyote yule lazima afirikie namna ambavyo nchi yake inaweza kujikomboa kiuchumi. Kisiasa tayari, mkoloni aliondoka."

Aidha, amebainisha kuwa,Serikali ya Tanzania inaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa maendeleo wa kimataifa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, huku akisisitiza kuwa ushirikiano huo umeendelea kuimarika licha ya changamoto za kimataifa za kifedha.

Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho kumekuwepo mijadala kuhusu athari za matukio ya kisiasa ya Oktoba,2025 kwa uhusiano wa Tanzania na jumuiya ya kimataifa.

Hata hivyo, Balozi Possi amesisitiza kuwa, Tanzania imeendelea kuwasilisha hoja na maelezo yake katika majukwaa ya kimataifa kwa uwazi na kuzingatia misingi ya kisheria na kidiplomasia.

Pia,ametoa wito kwa umma kupuuza taarifa zisizo na uthibitisho kuhusu madai ya kujiondoa kwa mashirika ya kimataifa, akisisitiza kuwa ushirikiano wa Tanzania na Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wengine wa maendeleo unaendelea kama kawaida.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here