NA DIRAMAKINI
MKUU wa Jeshi la Polisi, Camillus M.Wambura, amefanya mabadiliko madogo ya kiuongozi ndani ya Jeshi hilo kwa lengo la kujaza nafasi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro (RPC) iliyokuwa wazi.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 26,2026 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP),David Misime.Nafasi hiyo ilibaki wazi kufuatia uteuzi wa Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, aliyempandisha cheo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Alex Mkama kuwa Kamishna wa Polisi (CP) na kumteua kushika wadhifa wa Kamishna wa Polisi Jamii.
Katika mabadiliko hayo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Andrew Kantimbo amehamishwa kutoka Mkoa wa Mbeya alipokuwa akihudumu kama Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO), na sasa atachukua nafasi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa, mabadiliko hayo ni sehemu ya hatua za kawaida za kiutawala zinazolenga kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za usalama kwa wananchi.