DODOMA-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini leo Machi 26, 2026 imepitisha randama ya Wizara ya Madini kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka wa fedha 2026/27 katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma, ambacho pia kimepokea taarifa ya utekelezaji wa Wizara kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026 kwa mwaka 2025/26.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Subira Mgalu, ameipongeza Wizara kwa namna inavyosimamia utekelezaji wa majukumu yake yaliyopelekea kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa kufikia asilimia 12.7 katika robo ya tatu ya Julai hadi Septemba,2025 ikiwemo kuibua miradi mipya na shughuli za utafiti, na kueleza kwamba matokeo ya mchango wa Sekta ya Madini kwenye maendeleo na uchumi wa nchi yanaonekana dhahiri.


Pia ameipongeza Wizara kwa namna inavyodhibiti utoroshaji wa madini na biashara haramu ya madini nchini, hatua ambayo imepelekea kukamatwa kwa madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya shilingi trilioni 2.190 katika matukio 41 kwenye mikoa ya kimadini ya Arusha, Chunya, Geita, Dar es Salaam, Mwanza, Iringa, Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Kahama, Mahenge, Mbeya, Mbogwe, Mirerani na Songwe.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka 2025/26, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Madini, Augustino Olal, ameieleza kamati kuwa thamani ya mauzo ya madini na bidhaa za madini nje ya nchi mwaka 2024 ilikuwa dola za Marekani milioni 4,119.9 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 3,551.4 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 16.0, na kueleza kuwa “mauzo hayo yamechangia asilimia 57.0 ya mauzo yote ya bidhaa zisizo za asili nje ya nchi.”
Pia ameieleza kamati hiyo kuwa makusanyo ya maduhuli yaliyokusanywa na kuwasilishwa Hazina kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026 yameongezeka hadi kufikia shilingi 880,711,819,180.04 ikilinganishwa na shilingi 690,757,642,936.80 katika kipindi kama hicho mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 27.50. Mwaka 2025/26 Wizara imepangiwa kukusanya shilingi trilioni 1.2.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), amesema limesaini mkataba wa kuendeleza leseni za madini ya dhahabu zilizopo eneo la Kigosi, wilayani Bukombe mkoani Geita, na Kampuni ya Plantcor Mining and Plant Hire (PTY) Ltd ya nchini Afrika Kusini.
Ameongeza kuwa STAMICO imepata mikataba ya uchorongaji katika Kampuni ya GFX yenye thamani ya shilingi bilioni 3.8 na Shanta Buhemba yenye thamani ya shilingi bilioni 1.4.
“Mhe. Mwenyekiti, katika kipindi husika jumla ya leseni 9,802 zilitolewa, ikiwa ni zaidi ya lengo la leseni 6,687 zilizopangwa kutolewa, sawa na asilimia 146.58,” amesema Olal.
Akizungumzia mafanikio ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), ameyataja baadhi, ikiwemo maabara ya taasisi hiyo kukidhi vigezo vya kuendelea kuwa na ithibati (maintained accreditation status) kwa kipindi kingine cha miaka mitano (5) mpaka Oktoba 2029, baada ya ukaguzi wa nje kupitia Shirika linalodhibiti ubora wa huduma za maabara katika nchi zilizopo Kusini mwa Bara la Afrika (SADCAS) uliofanyika Februari 24, 2026.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali katika kikao hicho, ameihakikishia kamati kuhusu kutekelezwa kwa mipango yote iliyopangwa na Wizara, ikiwemo ununuzi wa helikopta kwa ajili ya shughuli za utafiti, na kuishukuru kwa namna inavyoisimamia Wizara, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na maelekezo na usimamizi mzuri wa kamati hiyo.


















