GEITA-Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo akiwa na Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, ASF Keneth Mwakasitu wamefuatilia kwa karibu zoezi la ufukuaji kufuatia kuporomoka kwa maduara manne katika Mgodi wa Dhahabu wa Msasa uliopo wilayani Bukombe.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 29, 2026 SACP Safia Jongo ametoa taarifa ya tukio hilo na kusisitiza kuwa, hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokana na ajali hiyo.Aidha, ameeleza kuwa Jeshi la Polisi limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo ili kuzuia uhalifu na kulinda usalama wa raia pamoja na mali zao.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, ASF Keneth Mwakasitu, amesema zoezi la utafutaji linaendelea kufanyika kwa weledi mkubwa kwa kushirikiana na wananchi, ambapo tayari baadhi ya mali zilizokuwa zikitumika katika shughuli za uchimbaji zimepatikana.
Naye Chifu Mkuu wa Mgodi wa Msasa, James Nkamba ameeleza kuwa,zoezi hilo linaendelea vizuri, huku juhudi zikielekezwa katika kuhakikisha mali zote zilizofukiwa zinapatikana na kuhakikisha usimamizi katika eneo hilo ili kulinda maisha ya watu na mali zao na kuendesha shughuli za uchimbaji katika salama mkubwa.



