Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijisia kunufaisha wananchi 41,000 Zanzibar

ZANZIBAR-Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Balozi Mhandisi Zena Ahmed Said amesema, jumla ya wanufaika 41,000 kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii wanatarajia kunufaika na Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijisia unaotekelezwa na Wizara ya Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Balozi Mhandisi Zena Ahmed Said (wa pili kulia ) akizindundua Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania (PAMOJA), hafla ya uzinduzi imefanyika jana katika Ukumbi wa Chuo cha Polisi Zanzibar, wa pili kushoto ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mheshimiwa Anna Athanas Paul, na kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abeida Rashid Abdallah na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (TZ),Dkt. John Jingu (wa kwanza kulia).

Pia,amesema kupitia mradi huo utawawezesha kupata elimu na mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa biashara kabla ya kuanza kupatiwa mikopo.

Balozi Zena ameyasema hayo jana katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo Polisi Zanzibar Ziwani.

Amesema,wanufaika hao kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii wanatarajia kunufaika na Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijisia.
Amesema kwamba, huduma za Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto zitatolewa ili kuwapa fursa wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika shughuli zao za uzalishaji huku watoto wao wakiwa katika mazingira salama yatakayowaepusha na masuala ya udhalilishaji.

Balozi Zena amesema,Serikali inatambua kwamba masuala ya ukatili na udhalilishaji yamekuwa yakirudisha nyuma maendeleo ya nchi. Lakini Serikali imeanza kutayarisha bajeti kwa kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia (Gender Budgeting).
Amesema,mradi huo utaongeza nguvu katika kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji hasa kwa akina mama na watoto kwa kuimarisha miundombinu ya upatikanaji wa huduma kwawaathirika wa masuala ya udhalilishaji.

Ameeleza kwamba,Maendeleo ya Jamii hayapatikani ikiwa wananchi wanakabiliwa na misongo ya mawazo na afya ya akili,kwani Ustawi wa akili ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu katika kukabiliana na changamoto hizo.
Amesema,mradi huo unalenga kutoa huduma za kisaikolojia kwa waathirika wote wa vitendo vya udhalilishaji pamoja na wanajamii kwa ujumla kupitia kituo kitakachojengwa mahsusi kwa shughuli hizo, kitatoa huduma za ushauri nasaha kwa waathirika hao ambapo ushauri huo utasasaidia kuwarudisha katika hali zao za kawaida na kuimarisha ustawi wao.

Pia,amesema vituo vya malezi ya kutwa vitajengwa na baadhi ya majengo kukarabatiwa katika kuhakikisha suala la mama anashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na mtoto akilelewa katika mazingira salama, ikiwa ni njia moja wapo wa kusatawisha ustawi wa mtu mmoja mmoja.

Ameeleza,mradi katika utekelezaji wake utaratibu, utasimamia na kufuatilia masuala ya kupambana na udhalilishaji ikiwa ni sehemu ya jitihada zinazoendelea katika kuhakikisha utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Kupambana na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto wa Awamu ya Pili (NPA-VAWC II).
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Abeida Rashid Abdalla amesema, Mradi wa PAMOJA umeanzishwa ikiwa ni matokeo ya Jitihada za viongozi wakuu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Amesema, hatua hiyo ilitokana na mazungumzo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Benki ya Dunia ambapo katika mazungumzo hayo Benki ya Dunia ilipokea ombi la Mheshimiwa Rais kuhusiana na uanzishwaji wa mradi huo.

Ameeleza kwamba, Mradi wa PAMOJA unatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar ambapo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (TZ) na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (ZNZ) zinaongoza utekelezaji kwa ujumla kutokana na majukumu yao na utaalamu katika ngazi ya Kitaifa na ni Mradi wa Miaka 5 na unatekelezwa na Wizara MJJWW kwa kushirikiana na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA).
Katibu Mkuu Abeida amesema,mikopo itakayoombwa ni kuanzia shilingi laki 5 hadi Milioni 30 na muda wa kurejesha ni kuanzia mwaka mmoja (miezi 12) hadi miaka 2 (miezi 24).

Kwa upande wa washiriki wa mkutano huo akizungumza, Zuhura Nassor amesema kikundi chao cha kiitwacho Faraja Yetu kimeshajisali, hivyo wanasubiri kuanza kupewa mikopo kwa ajili ya kuboresha bidhaa zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here