NA DIRAMAKINI
MTAALAMU wa usalama mtandao na uchunguzi wa makosa ya kidijitali, Yusuph Kileo ameshiriki mkutano wa kimataifa wa masuala ya teknolojia uliofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini, ambapo aliwasilisha mada kuhusu mchango wa usalama mtandao katika kukuza uchumi.
Katika mkutano huo, Kileo alikuwa miongoni mwa wazungumzaji wakuu (Keynote Speaker), akitoa mada iliyojikita katika namna uimarishaji wa mifumo ya usalama mtandao unavyoweza kuchochea ukuaji wa kiuchumi kwa kulinda miundombinu ya kidijitali, kuimarisha imani kwa wawekezaji, na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma na binafsi.
Akifafanua hoja zake, alieleza kuwa katika zama za mageuzi ya nne ya viwanda (Fourth Industrial Revolution), mataifa hayawezi kujenga uchumi imara bila kuwa na mifumo madhubuti ya kulinda taarifa, miundombinu ya mawasiliano, pamoja na majukwaa ya kidijitali yanayotegemewa na sekta mbalimbali.
Mbali na ushiriki wake katika mkutano huo, Kileo alipata fursa ya kupokelewa na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Anga la Afrika Kusini, Luteni Jenerali Wiseman Mbambo.
Mazungumzo yao yalijikita katika changamoto zinazoikabili sekta ya usafiri wa anga kufuatia ongezeko kubwa la matumizi ya teknolojia za kisasa katika uendeshaji wa vyombo vya anga na mifumo ya urambazaji (navigation).
Katika mazungumzo hayo, Kileo alielezea mbinu mbalimbali za kitaalamu zinazoweza kutumika kuimarisha usalama mtandao katika sekta ya anga, ikiwemo ulinzi wa mifumo ya mawasiliano, usimamizi wa taarifa nyeti, pamoja na mafunzo endelevu kwa wataalamu wa TEHAMA katika taasisi za ulinzi na usafiri wa anga.
Aidha,kwa kutambua mchango wake katika uwanja wa usalama mtandao na uchunguzi wa makosa ya kidijitali, Luteni Jenerali Mbambo alimkabidhi Kileo tuzo maalum kama ishara ya shukrani na kuthamini utaalamu wake.

Ushiriki wa Kileo katika mkutano huo unaendelea kudhihirisha nafasi ya wataalamu wa Afrika katika kujenga mazingira salama ya kidijitali, yanayowezesha maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii barani Afrika na duniani kwa ujumla.




