NA DIRAMAKINI
JUMLA ya watu 18 wamefariki dunia kufuatia maafa yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha leo Machi 25,2026 kati ya saa 6 hadi saa 9:30 usiku katika Kata ya Nkunga, Lupepo, Kawetele na Ikuti wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Benjamin Kuzaga amesema, kati ya waliofariki, watu wazima ni wanne (wanawake watatu na mwanaume mmoja) huku watoto wakiwa 14 (wa kike wanane na wa kiume sita).
SACP Kuzaga ametaja majina ya watu wazima waliopoteza maisha ni Chapakazi Mwasota (60), Rhoida Mwangwina (55), Gladness Chapakazi (18), Neema Mwasyema (31), Aneth Morohan (35), Obeid Shibuka (20) na Itika Manyanya (26).
Watoto waliofariki ni Vivian Ahonga (mwaka 1), Briana Mwachiombo (3), Dailan Kasambala (6), aliyekuwa mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya Msingi Lupepo, Innoent Kasambala (4), Vivian Andrea (13), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Lupepo.
Princess Ibrahim (5), aliyekuwa mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya Msingi Lupepo, Nathanael Christopher (2), Jonathan Hamis (miezi 10), Irine Anangisye (16), aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lupepo.
Wengine ni Wema Hamis (5) aliyekuwa mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya Msingi Kikuyu na Kenedy Mahenge (14), aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ikuti.
Amesema,maafa hayo yalisababishwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali, hali iliyosababisha maporomoko ya udongo mzito yaliyosomba nyumba zaidi ya tisa zilizojengwa kwa tofali za udongo na kuezekwa kwa mabati.
Aidha, watu watano walijeruhiwa, wakiwemo watoto watatu wa kike na watu wazima wawili (mwanaume mmoja na mwanamke mmoja).
Kamanda huyo amesema, majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Makandana, Tukuyu pamoja na Zahanati ya Chuo cha Magereza Kiwira.
Wakati huo huo,Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea na operesheni za uokoaji katika maeneo yaliyoathirika.
Vilevile, timu za wataalamu wa afya zinaendelea na uchunguzi wa kitabibu wa miili ya marehemu na kutoa huduma za awali kwa waathirika.
Kwa upande wake, Kamati ya Maafa ya Wilaya inaendelea na tathmini ya athari za tukio hilo pamoja na uratibu wa utoaji wa misaada kwa wananchi walioathirika.

