NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Gilbert Edwin Mwabulesi (26) mkazi wa Ibililo wilayani Rungwe kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi, Edwin Mwabulesi (65).
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Machi 25, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,SACP Benjamin Kuzaga amesema kuwa, mtuhumiwa anadaiwa kutekeleza tukio hilo kwa kumpiga baba yake sehemu mbalimbali za mwili hadi kusababisha kifo chake.Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, tukio hilo lilitokea Machi 21, 2026 majira ya saa 9:20 usiku katika Kitongoji cha Nsanga, Kijiji cha Ibililo, Kata ya Nkunga, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa, chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia kati ya mtuhumiwa na marehemu. Inadaiwa kuwa, mtuhumiwa ambaye alikuwa akiishi na wazazi wake, alirejea nyumbani usiku na kuanza kugonga mlango kwa nguvu huku akipiga kelele.
Kutokana na hali hiyo, baba yake aliamka na kumfuata kwa lengo la kumkanya, ndipo mtuhumiwa alipomshambulia kwa ngumi na mateke na kusababisha kifo chake.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa, linaendelea kukamilisha taratibu za kisheria ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua za masika zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.
Jeshi hilo limeongeza kuwa, linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa raia pamoja na mali zao kwa kuendesha misako na doria katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya, hatua inayolenga kudumisha amani na utulivu.