Mwanamke anapowezeshwa kifedha manufaa yake huenea kwa familia,jamii na taifa kwa ujumla-Naibu Gavana Msemo

DAR-Elimu ya fedha imeelezwa kuwa nyenzo muhimu katika kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kujenga ustahimilivu dhidi ya changamoto za kiuchumi.
Hayo yameelezwa leo Machi 4, 2026 na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Sauda Kassim Msemo, wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake lililofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Bi. Msemo alisema kuwa elimu ya fedha si maarifa ya nadharia pekee, bali ni daraja la uwezeshaji linalowasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi na kuwa washiriki hai katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Alisisitiza kuwa mwanamke anapowezeshwa kifedha, manufaa yake huenea kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Alieleza kuwa kauli mbiu ya kongamano hilo isemayo, “Miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania: Elimu ya Fedha kama Chachu ya Uwezeshaji na Ustahimilivu wa Wanawake Kiuchumi”, inaakisi dhamira ya taasisi hiyo katika kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wanawake wa makundi yote, wakiwemo wajasiriamali wadogo, wakulima, wafanyabiashara na wale walioko katika sekta isiyo rasmi.

Aidha, aliwataka wanawake kutumia taasisi za fedha zilizoidhinishwa na Benki Kuu wanapohitaji huduma za mikopo au bidhaa nyingine za kifedha.
Alisisitiza umuhimu wa kujiridhisha kuwa taasisi husika ina leseni halali, kusoma kwa makini masharti ya mkataba kabla ya kusaini, na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapobaini ukiukwaji wa sheria.

Bi. Msemo aliongeza kuwa Benki Kuu imeweka mifumo ya usimamizi kwa taasisi zinazotoa huduma za kifedha kwa utaratibu wa riba na pia zisizo za riba ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma rasmi zinazowiana na mahitaji na imani zao.
Washiriki wa kongamano hilo walipata fursa ya kujifunza kuhusu jukumu la BoT katika kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha na namna wanavyoweza kuwasilisha malalamiko yao kupitia mfumo wa Sema na BoT.

Aidha, walielimishwa kuhusu mbinu bora za usimamizi wa fedha binafsi, zikiwemo kupanga bajeti, kuweka akiba, kutumia mikopo kwa uwajibikaji na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha kwa ustawi wa muda mfupi na mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here