DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) wameshiriki katika hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi Mradi wa Ujenzi wa Matenki 15 ya Kupokea Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya mita za ujazo 378,000 za mafuta, liliwekwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 678.6 ni kichocheo kipya cha mapinduzi ya nishati na biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kupunguza muda wa meli za mafuta kukaa bandarini kutoka wastani wa siku 10 hadi siku tatu pekee, hivyo kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na mapato ya Serikali.









