Mwinjilisti Dkt.Temba ampongeza Mzee wa Upako na kusisitiza malezi ya kizazi kipya cha wahubiri nchini

DAR-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Dkt. Alphonce Temba amekutana na Mchungaji Anthony Lusekelo, maarufu kama Mzee wa Upako, katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya harusi na kutumia fursa hiyo kumpongeza kwa kudumu katika huduma ya injili kwa zaidi ya miaka 45.
Katika mazungumzo yao Machi 22,2026, Dkt. Temba alieleza umuhimu wa uzoefu wa Mchungaji Lusekelo katika kuongoza na kulea kizazi kipya cha watumishi wa Mungu, hususan vijana wa kizazi cha Gen Z, ambao kwa sasa wanatumia kwa kiasi kikubwa majukwaa ya mitandao ya kijamii kuhubiri injili.

Alisisitiza kuwa, kutokana na heshima na ushawishi alionao Mzee wa Upako ndani na nje ya mitandao ya kijamii, ana nafasi ya kipekee ya kusaidia kuwaongoza vijana hao ili wafanye kazi ya Mungu kwa nidhamu, maadili ya Kibiblia na uwajibikaji wa kiroho.

“Tunahitaji mtu mwenye uzoefu, uwezo na ujasiri. Kwa sasa hapa Tanzania, Mzee wa Upako ni miongoni mwa watumishi wanaoweza kusaidia vijana wanaohubiri kupitia mitandao kufuata maadili na misingi sahihi ya injili,” alisema Dkt. Temba.

Aidha, alisisitiza kuwa kazi ya injili inapaswa kujengwa juu ya misingi ya kuheshimiana, kuvumiliana na kusameheana, akibainisha kuwa injili haina nafasi ya visasi wala migogoro isiyo na tija.
Katika hatua nyingine, Dkt. Temba alitoa rai kwa Mchungaji Lusekelo kuwashirikisha watumishi wa Mungu wa rika mbalimbali, wakiwemo wale wanaokumbwa na migogoro ya mara kwa mara, ili kusaidia kurejesha utulivu ndani ya kanisa.

Alionya kuwa baadhi ya watumishi wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kushambuliana, jambo linalochafua taswira ya kanisa na kupotosha waumini, hususan vijana.

Alieleza kuwa,mwenendo huo unasababisha mkanganyiko kuhusu maana halisi ya utumishi, uvumilivu na hofu ya Mungu, huku ukilitia doa kanisa mbele ya jamii.

“Kwa sasa, mtu yeyote anaweza kutafuta umaarufu kupitia mitandao kwa kuwatukana watumishi wa Mungu, viongozi wa dini nyingine au hata Serikali, hali ambayo ni kinyume na maadili ya kiroho na mafundisho ya Biblia,” aliongeza.

Dkt. Temba pia alipendekeza kuanzishwa kwa jukwaa maalum litakalowakutanisha watumishi wa Mungu kwa ajili ya kujadiliana changamoto, kushauriana na kuweka miongozo ya nidhamu na maadili katika utumishi.

Alifafanua kuwa, jukwaa hilo linaweza kusaidia kuimarisha umoja wa kanisa na kutoa suluhisho la migogoro ya ndani.

Akitoa mfano wa Kibiblia, alirejea namna nabii Musa alivyoshauriwa na baba mkwe wake kuhusu mfumo bora wa uongozi, uliosaidia kugawanya majukumu na kuongeza ufanisi-mfumo unaofanana na utawala wa kisasa wenye ngazi mbalimbali za uongozi serikalini.

Kwa mujibu wa Dkt.Temba, ipo haja kwa watumishi wa Mungu kurejea kwa wazee wa kiroho wanapokumbwa na changamoto mbalimbali, ili kupata hekima na mwelekeo sahihi, hatua itakayosaidia pia kutatua migogoro ya kifamilia na ndoa miongoni mwa watumishi.Kwa upande wake, Mchungaji Anthony Lusekelo alimshukuru Dkt. Temba kwa maono na ushauri wake, akieleza kuwa anamfahamu kwa muda mrefu na amekuwa akifuatilia huduma yake ndani na nje ya nchi.

Alibainisha kuwa,kwamba licha ya kupita zaidi ya miaka 15 bila kukutana, ameendelea kushuhudia kazi nzuri anayofanya.

Mchungaji Lusekelo alisema, amepokea ushauri wa kuanzishwa kwa jukwaa hilo kwa mikono miwili na kuahidi kuufanyia kazi kwa lengo la kuondoa migogoro isiyo ya lazima ndani ya kanisa, pamoja na kudhibiti usambazaji wa masuala ya ndani ya watumishi katika mitandao ya kijamii.

Alisisitiza kuwa,hatua hiyo itasaidia kulinda heshima ya kanisa na kuimarisha kazi ya Mungu katika jamii.

Miongoni mwa sifa kuu za Mchungaji Mzee wa Upako ni kwamba, ingawa anastahili kuitwa Askofu au hata Daktari kutokana na wito wake na mchango wake mkubwa katika huduma ya kiroho, hapendi kabisa kuitwa kwa vyeo hivyo. 

Hapendezwi na heshima za udaktari wala kuitwa Askofu Anthony Lusekelo. Hali hii inaonesha unyenyekevu wa hali ya juu kwa kiongozi wa kiimani ambaye ametenda kazi kubwa na kujipatia heshima kubwa ndani na nje ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here