NEW DELHI-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe amekutana na wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini India katika mkutano uliolenga kusikiliza maoni yao, kujadili changamoto wanazokutana nazo pamoja na kuhimiza mchango wao katika maendeleo ya taifa. 

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Machi 8, 2026 kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini New Delhi, Mhe. Dkt. Maghembe aliwahimiza wanafunzi hao kutumia kikamilifu fursa ya elimu wanayoipata nchini India kwa kujifunza kwa bidii na kujijengea ujuzi wa kisasa utakaochangia maendeleo ya Tanzania baada ya kuhitimu masomo yao.
Alisema, Serikali inatambua umuhimu wa vijana wanaosoma nje ya nchi katika kuleta maarifa mapya, teknolojia na ubunifu unaoweza kusaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Akiwaeleza kuhusu hali ya nchi alisema hali ya nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kujenga Taifa kama kawaida.
Pia aliongeza kusema, Serikali imeendelea kulipa kipaumbele suala la vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa na kwamba tayari imeanzisha Wizara mahsusi kwa ajili ya kusimamia masuala ya vijana ambayo ipo chini ya Ofisi ya ya Rais.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaasa na kuwahimiza wanafunzi hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania nchini India kwa kuzingatia maadili, sheria za nchi wanayosoma na kudumisha mshikamano miongoni mwao.
Awali akizungumza kumkaribisha Mhe Naibu Waziri, Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Anisa Mbega aliwapongeza Wanafunzi hao kwa ushirikiano wanaotoa kwa ubalozi wakati wote pamoja na kudumisha sifa nzuri ya Tanzania ya umoja na mshikamano.
Kwa upande wa wanafunzi ambao waliwakilishwa na Rais wa Jumuiya yao ya TANSIN, Bw. Jumbe Juma Kawanza walimshukuru Naibu Waziri kwa kutenga muda na kukutana nao, wakisema hatua hiyo imewapa moyo na kuwafanya wajione kuwa sehemu ya juhudi za maendeleo ya Tanzania hata wakiwa nje ya nchi. Pia waliahidi kusoma kwa bidii ili kutoa mchango chanya kwa Taifa.Mhe. Dkt. Maghembe alikuwa nchini India kwa ziara ya kikazi pamoja na kushiriki Mkutano wa Jukwaa la Raisina 2026 kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Kombo.











