NEW DELHI-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe ameshiriki katika hafla ya ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Majadiliano wa Raisina 2026 (Raisina Dialogue) uliofanyika jijini New Delhi, India, Machi 5, 2026.
Hafla ya ufunguzi iliongozwa na Rais wa Finland ambaye pia alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo, Mhe. Alexander Stubb. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Stubb alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na kutumia mazungumzo kama nyenzo muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya haraka katika mazingira ya kisiasa duniani.Alieleza kuwa ni muhimu kwa mataifa kushirikiana katika kushughulikia changamoto za pamoja za kimataifa kama vile usalama, mageuzi ya kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya teknolojia.
Aidha, Waziri Mkuu wa India na Mwenyeji wa mkutano huo, Mhe. Narendra Modi naye pia alishiriki.
Aidha, mbali na kuhudhuria ufunguzi huo, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe alialikwa kushiriki hafla maalum ya chakula cha jioni ikiwa ni sehemu ya ufunguzi wa Majadiliano ya Jukwaa la Raisina 2026 iliyofanyika Machi 5, 2026 jijini New Delhi.
Majadiliano hayo yaliyobeba mada isemayo “The Global Crossroads: Assertion, Accommodation, Advancements yalifunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa India, Mhe. Vikram Misri na kuhudhuriwa na Mawaziri, wanadiplomasia na wataalam wa masuala ya kimkakati kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Aidha, wakati wa mkutano huo, Mhe.Dkt. Maghembe alipata nafasi ya kusalimiana na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya na Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri, Mhe. Musalia Mudavadi.
Kwenye Mkutano huo, Mhe. Dkt. Maghembe aliongozana na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Felista Rugambwa.
Mhe. Dkt. Maghembe yupo nchini India kwa ziara ya kikazi pamoja na kushiriki Mkutano wa Jukwaa la Raisina 2026 kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Raisina Dialogue ni mkutano wa kimataifa unaofanyika kila mwaka nchini India. Mkutano huo huwaleta pamoja viongozi wa serikali, wanadiplomasia, wanazuoni, wanajeshi, wafanyabiashara na wataalam wa sera kutoka duniani kote kujadili masuala ya siasa za kimataifa na usalama.
Mkutano wa Raisina huandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje ya India na taasisi ya Observer Research Foundation (ORF) ya nchini humo.









