NA GODFREY NNKO
BENKI ya NMB imelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa juhudi zake za kuendeleza miradi ya ujenzi wa nyumba bora na za kisasa zinazolenga kuboresha makazi na fursa za biashara kwa Watanzania.
Muonekano wa moja ya jengo la Mradi wa 7/11 (kulia) ambao umetembelewa na maafisa masoko kutoka NMB leo na ujenzi unaendelea, kushoto kwa mbali unaonekana Mradi wa NHC wa Samia House Scheme Phase I ambao tayari umekamilika katika eneo la Tanganyika Packers lililopo Kawe jijini Dar es Salaam.Pongezi hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Meneja Mawasiliano wa Mikopo ya Nyumba wa Benki ya NMB, Pauline Sangale, kufuatia ziara ya maafisa 30 kutoka Idara ya Masoko ya benki hiyo waliotembelea miradi miwili ya makazi inayotekelezwa na shirika hilo.
Miradi iliyotembelewa ni Samia House Scheme Phase II uliopo Kijichi pamoja na mradi wa 7/11 uliopo Kawe, jijini Dar es Salaam.Akizungumza baada ya ziara hiyo, Sangale amesema, ujumbe huo umeridhishwa na ubora wa nyumba zinazojengwa na NHC, akibainisha kuwa miradi hiyo inaendana na viwango vya kisasa vya makazi.
“Tumeona kazi kubwa iliyofanyika. Nyumba ni nzuri na zina ubora wa hali ya juu. Tunawahimiza Watanzania kuchangamkia fursa ya kumiliki nyumba katika miradi hii,” amesema Sangale.
Ameongeza kuwa Benki ya NMB iko tayari kuwawezesha Watanzania kumiliki nyumba hizo kupitia mikopo ya nyumba inayoweza kufikia hadi asilimia 90 ya thamani ya nyumba.
“Wananchi wasiwe na hofu kuhusu bei ya nyumba. Kupitia NMB, tunaweza kutoa mkopo wa hadi asilimia 90 ya thamani ya nyumba, hivyo kumwezesha Mtanzania kumiliki makazi bora kupitia miradi ya NHC,” amesema.
Ujumbe wa Maafisa Masoko wa NMB wakiwa katika Mradi wa Samia House Scheme Phase II uliopo Kijichi ambapo ujenzi unaendelea.
Sangale pia amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa mchango wake katika kuboresha sekta ya makazi nchini kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa katika maeneo tofauti ya Tanzania.Aidha, amesema ni jambo la faraja kuona Watanzania wanapata nyumba zenye ubora na hadhi kubwa kulingana na thamani ya fedha wanazowekeza kupitia miradi ya shirika hilo.
“Hivyo tunawahamasisha wateja wetu na Watanzania kwa ujumla kutembelea miradi hii ya NHC ili kujionea wenyewe ubora wa nyumba hizo na kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji kwa manufaa ya sasa na ya baadaye,” ameongeza.
Kwa upande wake, Afisa Mauzo wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoani Dar es Salaam, Thobias Kavishe, amesema ujio wa ujumbe wa NMB ni muhimu kwa kuwa benki hiyo ni miongoni mwa taasisi za kifedha washirika katika kuwezesha mauzo ya nyumba zinazojengwa na shirika hilo.
Kavishe amesema miradi iliyotembelewa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa miaka 10 wa shirika hilo unaolenga kujenga jumla ya nyumba 10,000 nchini.Akizungumzia Mradi wa Samia House Scheme Phase II uliopo Kijichi, Kavishe amesema mradi huo unajumuisha majengo 12 yenye jumla ya nyumba 260.
Ameeleza kuwa ujenzi wa mradi huo unaendelea kwa kasi na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Kuhusu Mradi wa 7/11 uliopo Kawe, amesema unatarajiwa kukamilika mwaka huu na unajumuisha majengo nane yenye ghorofa 17 kila moja.
Ameongeza kuwa kupitia mradi huo, jumla ya nyumba 420 zitapatikana, huku ukiwa ni mradi wa kisasa unaojumuisha huduma mbalimbali za makazi na biashara zinazomwezesha mkazi kuishi katika mazingira yenye hadhi ya juu.
“Tunaendelea kuwakaribisha Watanzania kuja kuwekeza katika miradi hii ya shirika, ambayo inatoa fursa mbalimbali za kumiliki nyumba au kuwekeza katika sekta ya makazi,” amesema.Kavishe ameongeza kuwa wananchi wanaweza kumiliki nyumba hizo kupitia njia tatu za malipo, ambazo ni kulipa fedha taslimu, kupata mkopo kupitia benki washirika au kulipa kidogo kidogo hadi mradi utakapokamilika.




