NA GODFREY NNKO
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Masanja Kadogosa imehairisha ziara yake ya kukagua miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) iliyopo jijini Dar es Salaam kufuatia kupokea taarifa za kifo cha Mbunge wa Jimbo la Isimani, Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi.
Taarifa za kifo cha Mheshimiwa Lukuvi, ambaye pia alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), zimeifikia kamati hiyo wakati tayari ikiwa imeshakamilisha ukaguzi wa Mradi wa Samia House Scheme Awamu ya Kwanza uliopo eneo la Tanganyika Packers, Kawe.
Mradi huo unaojumuisha majengo ya ghorofa 10 yenye jumla ya nyumba 560, umekamilika na tayari baadhi ya wanunuzi wamehamia na wengine kupangisha.
Hata hivyo, kamati hiyo haikuweza kuendelea na ukaguzi katika Mradi wa 7/11 uliopo Kawe baada ya kupokea taarifa hizo za msiba.
Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, Mwenyekiti wa PIC, Mheshimiwa Kadogosa, amesema, kwa mujibu wa taratibu za kibunge, shughuli za kamati zinapaswa kusitishwa pindi linapotokea tukio la kifo cha Mbunge.
“Kwa kuzingatia taratibu za kibunge, pamoja na kwamba tupo katika ziara ya kikazi, tunapopokea taarifa za msiba wa Mbunge mwenzetu na aliyekuwa Waziri, tunalazimika kuahirisha shughuli zetu. Hivyo, ziara hii inaahirishwa hadi kesho,” amesema Mheshimiwa Kadogosa.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 176 ya Kanuni za Kudumu za Bunge ya mwaka 2025, endapo Mbunge atafariki dunia wakati Bunge likiwa linaendelea na shughuli zake, Spika anapaswa kuahirisha shughuli za Bunge kwa siku hiyo.
Aidha,kutokana na kamati kuwa sehemu ya Bunge, uongozi wa kamati hiyo umeona ni busara kuahirisha ziara ili kupisha maombolezo.
Aidha, Mwenyekiti huyo alitangaza kuahirishwa kwa vikao vyote vya kamati kwa siku ya leo huku akibainisha kuwa, wabunge watapewa mwongozo wa hatua zinazofuata kuhusiana na msiba huo.
Kamati hiyo pia imetoa salamu za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia kifo cha Mheshimiwa Lukuvi aliyekuwa miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri.
Vilevile, imetoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wananchi wa Jimbo la Isimani kwa kuondokewa na kiongozi wao aliyewahudumia kwa muda mrefu na kuchangia maendeleo ya Taifa.
NHC yaomboleza
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah amesema, shirika hilo limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo hicho kilichotokea wakati wa ziara ya kamati hiyo.
“Kwa niaba ya Shirika la Nyumba la Taifa, tunatoa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Spika wa Bunge, pamoja na familia ya marehemu kwa kumpoteza kiongozi mahiri aliyelitumikia Taifa kwa uadilifu,”amesema Bw.Abdallah.Ameongeza kuwa,marehemu Lukuvi aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambapo alisimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa 7/11 uliokusudiwa kukaguliwa na kamati hiyo leo.
“Tumempoteza kiongozi aliyekuwa na maono makubwa ya kuleta mageuzi katika sekta ya makazi na maendeleo ya miji. Hakika pengo lake ni kubwa."
Mkurugenzi Mkuu huyo ameeleza kuwa, shirika hilo linaungana na Watanzania wote kumuombea marehemu apumzike kwa amani, huku akitoa pole kwa wote walioguswa na msiba huo.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Ikulu leo, Mheshimiwa Lukuvi amefariki dunia majira ya saa moja asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu kufuatia maradhi ya mshtuko wa moyo.
Tags
Breaking News
Bunge la Tanzania
Habari
Kamati ya Bunge
Kamati ya PIC
NHC Tanzania
Samia Housing Scheme Kawe
Seven Eleven 711 Kawe
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)

