ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo la Ismani na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. William Vangimembe Lukuvi (Mb.).
Katika salamu zake alizozitoa leo Machi 25, 2026, Rais Dkt. Mwinyi amesema, amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo hicho, akieleza kuwa Taifa limepoteza kiongozi shupavu aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Ameeleza kuwa, marehemu Lukuvi atakumbukwa kwa uongozi wake thabiti, uzalendo uliotukuka na kujitolea kwake kwa muda mrefu katika kulitumikia Taifa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametoa pole za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, familia ya marehemu, ndugu, jamaa pamoja na Watanzania wote kwa msiba huo mzito.
"Nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa kwa Taifa, uongozi wake thabiti na uzalendo wake uliotukuka katika kulitumikia Taifa kwa muda mrefu. Ninatoa pole za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa msiba huu mzito. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina."Rais Dkt.Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi na kuwapa faraja na subira wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu.