NA DIRAMAKINI
WANAFUNZI watatu wa Shule ya Msingi Msongola iliyopo Kata ya Msongola katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, wamefariki dunia kwa kupigwa na radi wakiwa katika mazingira ya shule wakicheza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyothibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, tukio hilo limetokea Jumatano, Machi 18, 2026, wakati wanafunzi hao walipokuwa wakicheza katika eneo la shule.
Kamanda Muliro amesema kuwa, jumla ya wanafunzi watano walikumbwa na mkasa huo, ambapo watatu walipoteza maisha papo hapo, huku wawili wakijeruhiwa na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.
“Ni kweli wanafunzi watano walikuwa wakicheza shuleni wakapigwa na radi; watatu walifariki papo hapo na wawili wanaendelea kupatiwa matibabu,” amesema Muliro.
Taarifa zaidi zimeeleza kuwa, tukio hilo limeacha huzuni kubwa miongoni mwa wakazi wa Msongola na Jimbo la Kivule, familia za marehemu pamoja na jamii ya shule kwa ujumla.
Viongozi na wadau mbalimbali wameungana na familia zilizopoteza wapendwa wao, wakitoa pole na kuwataka kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
Aidha,wataalamu wa hali ya hewa na usalama wamekuwa wakisisitiza kuwa wakati wa mvua, ni muhimu kuepuka maeneo ya wazi, miti mikubwa, na miundombinu isiyo salama ili kupunguza hatari ya kupigwa na radi.
