Rais Dkt.Mwinyi ateua viongozi mbalimbali

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amefanya uteuzi wa viongozi kadhaa katika taasisi muhimu za Serikali, hatua inayolenga kuimarisha ufanisi wa utendaji wa sekta mbalimbali za maendeleo visiwani humo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Uteuzi huo unahusisha wataalamu wenye uzoefu wa muda mrefu katika nyanja za uhandisi, mipango, ujenzi pamoja na usimamizi wa taasisi za umma.

Katika uteuzi huo, Mhandisi Widady Ali Hassan ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara Zanzibar. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa akihudumu kama Mkurugenzi katika kampuni binafsi, akiwa na uzoefu mpana katika masuala ya miundombinu.

Aidha, Mhandisi Makame Ali Makame ameteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Kabla ya hapo, alikuwa akikaimu nafasi hiyo, hali inayodhihirisha imani ya Serikali kwa utendaji wake.

Katika sekta ya ujenzi, Mhandisi Riziki Jecha Salim ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Wakala wa Majengo Zanzibar. Awali alikuwa akihudumu kama Mhandisi Mwandamizi katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, akijishughulisha na miradi mbalimbali ya maendeleo ya miundombinu.

Kwa upande wa usimamizi wa ununuzi wa umma, Ndugu Ali Hemed Ali ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma Zanzibar (ZPPRA). Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Afisa Mwandamizi wa Ununuzi na Msimamizi wa Mfumo wa Ununuzi wa Kielektroniki katika Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora.

Vilevile, Ndugu Aliyah Emanuel Juma ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Halali wa Biashara Zanzibar (ZFCC), akitoka katika nafasi ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo.Taarifa hiyo imeeleza kuwa uteuzi huo utaanza rasmi tarehe 01 Aprili, 2026.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here