KITWE-Rais wa Jamhuri ya Zambia Dkt. Haikande Hichilema amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi mbalimbali anazofanya katika kutekeleza Ajenda ya Mabadiliko ya Nishati (energy transition) Barani Afrika.
Rais Dkt. Hichilema alitoa pongezi hizo Machi 26, 2026 wakati anafunga mkutano wa 13 wa Kimataifa wa Madini na Nishati (ZIMEC) uliofanyika kwa siku mbili nchini Zambia.Dkt. Hichilema alisema kuwa, Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, mkakati uliopata msukumo mkubwa kutoka kwa Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Aliongeza kuwa, katika ukanda wa nchi za Kusini mwa Afrika Tanzania inatekeleza ushirikiano wa kimkakati na Zambia kwa vitendo kupitia sera rafiki na miradi ya miundombinu inayounganisha kanda nzima.
Dkt. Hichilema alipongeza kuhusu mpango wa wizara ya migodi na maendeleo a madini nchini Zambia kwa kuweka lengo la uzalishaji wa tani milioni 3 za madini ya shaba ifikapo mwaka 2030.Katika mkutano huo Naibu Waziri wa Madini nchini Tanzania Dkt.Steven Kiruswa alipata fursa ya kuwasilisha mada kuhusu kuimarisha shoroba za miundombinu ya kikanda ili kuongeza tija na ushindani wa kibiashara.


