Salamu za Jumapili: Ni yeye atakuokoa

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, katika nyakati hizi zenye changamoto nyingi za kiuchumi, kijamii na kimaadili, wanadamu wamejikuta wakitafuta majibu katika mifumo na mbinu mbalimbali za kibinadamu.
Hata hivyo, historia inatufundisha kuwa pamoja na juhudi zote za kisayansi na kiutawala, mwanadamu hubaki na mipaka yake. Ni katika upeo huo ndipo hoja kuu hujitokeza kwa uzito kuwa,ni Mungu pekee ndiye atatuokoa.

Aidha, kimaadili na kiroho, jamii inahitaji mwanga utakaorejesha matumaini, haki na mshikamano. Bila dira ya kiungu, misingi ya uadilifu na huruma hutikisika.

Tunaposhuhudia ongezeko la migogoro, mmomonyoko wa maadili na kukosekana kwa amani ya kweli, tunapaswa kutambua kwamba suluhu ya kudumu haiwezi kupatikana kwa nguvu za kibinadamu pekee, bali kwa kurejea katika chanzo cha uhai na hekima.

Imani kwa Mungu si wazo la kufariji nafsi tu, bali ni msingi wa matumaini na mabadiliko ya kweli. Imani humjenga mwanadamu kuwa na uwajibikaji, subira na upendo ikiwa ni maadili yanayoweza kuibadilisha jamii kwa upana wake.

Pale ambapo mwanadamu hushindwa, nguvu ya Mungu hudhihirika kwa namna isiyotarajiwa, ikirejesha matumaini na kuleta njia mpya za mafanikio.

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ni wakati wa kutafakari upya mwelekeo wetu kama jamii. Badala ya kutegemea hekima na nguvu zetu peke yake, tunapaswa kunyenyekea na kuomba mwongozo wa Mungu katika kila hatua.

Vilevile, maombi, toba na mshikamano wa kweli vinaweza kuwa chachu ya mageuzi tunayoyatafuta.Endelea;

1. Ni Mungu huyo anasema, ni wewe anakuambia,
Ulipo ulivyo simama, huku zidi kumwangalia,
Wowote uje uhasama, kutaka kukufanyizia,
Ni yeye atakuokoa, ni yeye atakukomboa.

2. Mkono wa watu wabaya, ambao wakusarandia,
Lengo ni utendwe mabaya, ifikie kuangamia,
Usije kushika taya, kama ndiyo unaishia,
Ni yeye atakuokoa, ni yeye atakukomboa.

3. Mkono waja unatisha, kwa mbali kukusukumia,
Lengo lake kukuzimisha, tusije tukakusikia,
Muumba anathibisha, wewe huwezi kutitia,
Ni yeye atakuokoa, ni yeye atakukomboa.

4. Mungu ndiye Muweza yote, akilini ikuingia,
Kwa hiyo anaweza yote, hakuna linalosalia,
Kwa mashambulizi yoyote, Mwenyezi atakukingia,
Ni yeye atakuokoa, ni yeye atakukomboa.

5. Kwa hiyo kwa Mungu tumika, maisha ukifurahia,
Kwa vile unayo hakika, mabaya anakukingia,
Ni kazi bila ya mashaka, wala kuzimiazimia,
Ni yeye atakuokoa, ni yeye atakukomboa.

6. Ole kwa wakuchokozao, wewe wangekuangalia,
Wajue si saizi yao, wasije wakaangamia,
Kwa vile ulinzi unao, siyo wa hii dunia,
Ni yeye atakuokoa, ni yeye atakukomboa.
(Yeremia 15:21)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here