Sekta ya Maji yarekodi mafanikio chanya

MOROGORO-Sekta ya Maji imepongezwa kwa mafanikio yaliyopatikana kwa utekelezaji wa miaka ishirini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ametoa pongezi hizo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mapitio ya Pamoja ya Sekta ya Maji, ulioandaliwa na Wizara ya Maji, mjini Morogoro ikiwa ni sehemu ya Kuelekea Siku ya Maji Duniani Machi, 22.

Balozi Khamis amesema, Wizara ya Maji imetekeleza Progamu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) kwa ufanisi mkubwa tangu ilipozinduliwa mwaka 2006, ambapo upatikanaji wa huduma ya maji mjini ilikua asilimia 74 na vijijini ilikua ni asilimia 54, ukilinganisha na hali ya sasa ya upatikanaji wa maji nchini ambapo imefika asilimia 92.5 kwa mjini, na asilimia 85.2 kwa vijijini.

Amesema mkutano huo ni jukwaa la ngazi ya juu la majadiliano na tathmini ya utekelezaji wa WSDP.
Mhe. Balozi Khamis amesema " Mkutano huu ni maalumu kwa ajili ya kupokea taarifa ya hali ya Sekta ya Maji kwa kipindi cha Januari hadi Disemba 2025. Katika kipindi hicho jumla ya Shillingi Bilioni 883.93 sawa na Dola za Marekani milioni 351.04 zilipatikana kutoka kwa wadau wa maendeleo na vyanzo vya ndani vya serikali, fedha izo zilitumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maji na usafi wa mazingira".

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema, Serikali ya awamu ya sita imejipanga kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji nchini inafika asilimia mia moja.
Amesema hadi sasa vijiji 10,758 tayari vimeshapata huduma ya maji ya uhakika, na vijiji 1,575 kati ya vijiji 12,333 bado havijafikiwa na huduma ya maji ya uhakika na serikali itahakikisha vijiji vyote vinafikiwa na huduma ya maji ya uhakika kwa sababu tayari serikali imeanza kutekeleza miradi mikubwa ya maji na mkakati ikiwemo mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji.

Mhandisi Mwajuma amesema, lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Maji ili kwa pamoja waweze kupitia utekelezaji wa WSDP awamu ya tatu kwa kipindi cha Januari hadi Disemba 2025.
"Mkutano huu utajadili mafanikio na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa programu na kuweka mikakati ya utatuzi," Mhandisi Mwajuma amesema.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Mhe. Kigoma Adam Malima amemshukuru Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) na watendaji wa Wizara ya Maji kwa kufanya maadhimisho ya wiki ya maji Mkoani Morogoro.

Amesema "mkoa wa Morogoro ni mdau mkubwa wa Sekta ya Maji na unatambua wajibu wake wa kuhifadhi vyanzo vya maji, kwani mkoa huo ni chanzo kikuu cha maji kwa mikoa ya Dar es salaam na Pwani".

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here