NA DIRAMAKINI
SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana (OR-MV) imetangaza rasmi kufunguliwa kwa dirisha la kupokea maombi ya mikopo kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha vijana kiuchumi na kukuza ajira nchini.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa mpango wa mikopo wenye thamani ya Shilingi bilioni 200 ulioanzishwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, unaolenga vijana, wanawake pamoja na watu wenye mahitaji maalum.Mpango huo unatarajiwa kuchochea maendeleo ya ujasiriamali na kuongeza tija katika sekta mbalimbali za uzalishaji, biashara na huduma.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, vijana wote wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 wanahimizwa kuwasilisha maombi yao, wakiwa na miradi au mawazo ya miradi yenye tija.
Waombaji wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania wenye vitambulisho vya taifa (NIDA), wakaazi wa maeneo yanayotambuliwa kisheria kwa shughuli za kiuchumi, na kuthibitishwa na mamlaka za serikali za mitaa.
Aidha, waombaji wanaweza kuwa watu binafsi, kampuni changa au vikundi vya kijamii vilivyosajiliwa vinavyojihusisha na shughuli za uzalishaji mali.
Miongoni mwa vigezo vingine ni kuwa na andiko la mradi, akaunti ya benki au namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mwombaji.
Katika utaratibu wa uombaji, waombaji wanapaswa kuwasilisha barua rasmi ya maombi ikieleza jina la mwombaji au kikundi, aina ya mradi, kiasi cha mkopo kinachohitajika pamoja na eneo la utekelezaji wa mradi huo.
Nyaraka muhimu za kuambatisha ni pamoja na andiko la mradi lisilozidi kurasa tano, kitambulisho cha taifa au namba ya NIDA, namba ya mlipa kodi (TIN), leseni ya biashara kwa biashara zinazoendelea, pamoja na barua ya utambulisho kutoka serikali ya mtaa au kijiji.
Nyaraka nyingine ni picha mbili za hivi karibuni za mwombaji na, kwa vikundi, muhtasari wa kikao uliosainiwa na wanachama unaoidhinisha maombi ya mkopo.
Ofisi hiyo imeeleza kuwa maombi yote yanapaswa kuwasilishwa kwa njia ya barua pepe kupitia anuani rasmi ya mfuko kabla ya Aprili 3,2026.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana amesisitiza umuhimu wa vijana kutumia fursa hiyo kuboresha maisha yao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Tags
Fursa za Kiuchumi kwa Vijana
Habari
Mikopo kwa Vijana Tanzania
Mikopo ya Vijana
Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana
Vijana Tanzania

