ARUSHA-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa agizo la kukamatwa kwa Mkandarasi raia wa Iran wa Kampuni ya Tunnel Sade Ariana ambaye ameshindwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji la Eyasi lililopo Karatu mkoani Arusha.
Mkandarasi huyo ambaye mkataba wake umevunjwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ametakiwa kurejesha kiasi cha shilingi 3,274,794,302 kama malipo ya awali ya mradi huo.
Awali Mkandarasi huyo alikuwa na mkataba wa utekelezaji wa mradi wa shilingi Bilioni 21 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa na alikiuka makubaliano kwa kushindwa kutekeleza kazi, hivyo mkataba wake kuvunjwa.
Akizungumza mkoani Arusha wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi mwingine wa umwagiliaji upande wa skimu za Bonde la Eyasi unaotekelezwa na Mkandarasi M/S CRJE(EA),Waziri Mkuu amesema,atakula sahani moja na mkandarasi aliyekimbilia Mahakamani akiwa na fedha za Serikali.Hayo yalijiri baada ya Waziri Mkuu kupokea taarifa kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Karatu,Daniel Awack na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Umwagiliaji,Raymond Mndolwa kuwa mkandarasi huyo ametelekeza kazi na kuishtaki Serikali mahakamani huku akiwa bado anashikilia fedha za malipo ya awali.
Dkt.Mwigulu ameitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kushirikiana kwa karibu na mamlaka za vyombo vya dola, ikiwemo Idara ya Uhamiaji na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuhakikisha mkandarasi huyo anawajibika.
Pia,Waziri Mkuu amemuagiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kukamata hati ya kusafiria ya mkandarasi huyo ili asitoke nje ya nchi, akisisitiza kuwa kitendo cha kuchukua fedha za umma kisha kukimbilia mahakamani bila kutekeleza mradi ni dharau na hujuma ya wazi dhidi ya nchi.
"Unajua hawa watu wamekuwa na kiburi,mtu anaiba anakimbilia mahakamani. Zile ni hujuma, mambo ya aina hii ni dharau kwa nchi.
"Tumempa fedha hajatekeleza mradi, tunamwambia basi turudishie mradi wetu na fedha anaenda mahakamani. Fedha hajarudisha,vitu hajarudisha,anakimbilia mahakamani, hizi ni dharau sasa,"alisisitiza Dkt.Mwigulu.
"Na mimi hawa ndio nataka sometimes kushughulika na watu wa aina hii ataitapika hii fedha ya Serikali, nitahakikisha nakula naye sahani moja, akamatwe na azuiliwe kutoka nchini mara moja kokote alipo,”amesema.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Arusha, Mhandisi William Simon, amebainisha kuwa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 38.4 unalenga kuboresha mifereji ya asili na madakio yaliyotengenezwa kienyeji kwa mifuko ya mchanga na magogo, hali ambayo ilikuwa ikisababisha upotevu mkubwa wa maji na migogoro miongoni mwa wakulima.
Ametumia fursa hiyo kupongeza utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji inayoendelea ikiwemo skimu za Umwagiliaji Bonde la Eyasi ambapo ameweka jiwe la msingi.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa aliongeza kuwa, Serikali imeshatoa jumla ya shilingi bilioni 11.6 kwa mkandarasi huyo, kiasi ambacho kinajumuisha malipo ya awali ya zaidi ya shilingi bilioni 5.7.
Bw. Mndolwa amebainisha kuwa,baada ya vikao zaidi ya saba vya usuluhishi kushindwa kuzaa matunda na mkandarasi kuondoka eneo la mradi bila kufuata taratibu.
Amesema,tume ililazimika kuomba kibali kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuvunja mkataba huo. Kwa sasa, Serikali imezuia mitambo yote ya mkandarasi huyo iliyokuwa eneo la kazi kama sehemu ya hatua za kisheria za kurejesha fedha za umma zilizopotea.
Mhandisi Simon ameeleza kuwa, hadi kufikia Machi 2026, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 30, ambapo kazi zilizokamilika ni pamoja na kusakafia mifereji yenye urefu wa kilomita 24, ujenzi wa barabara za mashambani kwa kiwango cha changarawe kwa urefu wa kilomita 24.6, ujenzi wa ofisi ya meneja mradi, pamoja na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kugawa na kupunguza kasi ya maji.
Kukamilika kwa mradi huu ambao sasa unatazamiwa kufikia tamati ifikapo tarehe 2 Novemba 2026, kutarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa zaidi ya wakulima 2,500 katika skimu za Mang’ola Barazani, Maleckchand, Laghangareri, Mbuga Nyekundu, Jobaji na Dumbechand zenye jumla ya zaidi ya hekta 5,000.
Mhandisi Simon amehitimisha kwa kueleza kuwa mbali na maboresho ya mifereji, upo mpango wa ujenzi wa bwawa litakalosaidia kuongeza upatikanaji wa maji wakati wa kiangazi ili kuhakikisha kilimo cha Umwagiliaji kinaendelea kwa tija mwaka mzima.
Dkt. Mwigulu amewahakikishia wananchi kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haitawavumilia watu wanaochezea fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuwakomboa wakulima wa Karatu.














