Profesa Kabudi kuongoza ujumbe wa Tanzania katika mikutano ya Jumuiya ya Madola

LONDON-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Palamagamba Kabudi, amewasili jijini London, Uingereza kushiriki Kikao cha 72 cha Kamati ya Mawaziri wa Jumuiya ya Madola (CMAG) na Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo (CFAMM) utakaofanyika Machi 7, 2026 jijini London. Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo muhimu wa kimataifa unafuatia mwaliko rasmi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Shirley Botchwey.

Kikao hicho cha 72 cha CMAG kinalenga kufuatilia utekelezaji wa maamuzi na kuimarisha misingi na tunu za Jumuiya ya Madola ukiangazia masuala mbalimbali yanayohusu utawala bora, demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria miongoni mwa nchi wanachama 56 wa Jumuiya hiyo.
Aidha, Machi 8, 2026 Prof. Kabudi atashiriki Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola utakaofanyika jijini humo. Mkutano huo utajadili masuala ya kimkakati kuhusu mustakabali wa Jumuiya na namna ya kuimarisha mchango wake katika kukabiliana na changamoto za kimataifa.

Vilevile, mawaziri watajadili na kuweka mwelekeo wa vipaumbele vya sera kuelekea Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) utakaofanyika nchini Antigua and Barbuda Novemba 1 hadi 4, 2026, hatua inayolenga kuimarisha mshikamano na mageuzi ya Jumuiya katika mfumo wa kimataifa unaobadilika kwa kasi.

Katika mikutano hiyo, Prof. Kabudi anamwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ambapo pamoja na masuala mengine atawasilisha msimamo wa Tanzania katika ajenda mbalimbali zitakazojadiliwa na mawaziri wa nchi wanachama.
Katika ziara hiyo, Prof. Kabudi ameambatana na Mshauri wa Rais katika masuala ya Diplomasia, Balozi Lazaro Nyalandu. Wakiwa katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, wamepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Balozi Mbelwa Kairuki, ambaye amewasilisha taarifa kuhusu maandalizi na mwenendo wa mikutano hiyo ya Jumuiya ya Madola.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here