NA DIRAMAKINI
Ofisi ya Afisa Madini Mkazi – Mbogwe imetoa ufafanuzi rasmi kufuatia tukio la ajali ya kijiolojia lililotokea katika Mgodi wa Dhahabu wa Msasa uliopo Kijiji cha Msasa, Kata ya Runzewe, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, ambapo hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tukio hilo lilitokea Machi 29,2026 majira ya saa 4:00 asubuhi katika eneo linalojulikana kama Area A, baada ya kutokea kwa mpasuko wa ardhi ulioathiri maduara manne ya uchimbaji yenye namba KO 46A, 47A, 48A na 49A. Mpasuko huo ulisababisha sehemu ya maduara hayo kutitia ardhini.
Imeelezwa kuwa,maduara hayo yalikuwa tayari yamesimamishwa shughuli za uzalishaji tangu Machi 27, 2026 kufuatia maelekezo ya wakaguzi wa mgodi waliotaka yafanyiwe ukarabati wa kiusalama. Hali hiyo inaaminika kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa madhara kwa binadamu.
Chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, hali iliyosababisha kulegea kwa udongo na miamba katika eneo hilo la uchimbaji.
Mgodi wa Msasa, unaomilikiwa na wawekezaji binafsi wanne ambao ni Khadija Mkopi Mohamed, Amani Jackonia Mkaga, Boaz Lucas Nkise na Fadhili Victor Malema, una jumla ya leseni 17 za uchimbaji zilizotolewa Oktoba 22, 2025.
Tangu kuanza kwa shughuli zake kwa kasi mwezi Novemba 2025, mgodi huo umekuwa na takribani maduara 2,000 na kuvutia zaidi ya watu 20,000 wanaojihusisha na uchimbaji pamoja na shughuli za huduma.
Ofisi hiyo imebainisha kuwa wakati tukio linatokea hakukuwa na wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi katika eneo lililoathirika, kwani tayari walikuwa wameondolewa kwa ajili ya kupisha ukarabati uliopangwa.
Aidha, mfumo wa ukaguzi katika mgodi huo umeelezwa kuwa ni wa mara kwa mara, ukihusisha wakaguzi wapatao 200 wanaofanya kazi muda wote chini ya usimamizi wa karibu wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi – Mbogwe kwa kushirikiana na Mkaguzi Mkuu wa Migodi Tanzania pamoja na taasisi nyingine za Serikali.
Baada ya kubainika kwa dalili za hatari, hatua za haraka zilichukuliwa na wakaguzi wa mgodi kuwaondoa mafundi waliokuwa chini ya ardhi pamoja na watu waliokuwa karibu na eneo hilo, ambapo wote walifanikiwa kutoka salama.
Vikosi vya uokozi vilivyohusisha wataalamu kutoka ofisi za madini, zimamoto na uokoaji, Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama vilifika eneo la tukio kwa wakati na kusimamisha shughuli zote za uchimbaji kwa muda.
Hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuweka alama za tahadhari katika eneo lililoathirika na kudhibiti mkusanyiko wa wananchi waliokuwa wakijaribu kusogea karibu na eneo la hatari.
Kwa sasa, uchunguzi wa kina unaendelea kufanywa ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo na kuandaa mpango madhubuti wa ukarabati pamoja na mwendelezo salama wa shughuli za uchimbaji.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya timu ya uokozi, wakaguzi wa migodi na vyombo vya usalama, hakuna mtu aliyeripotiwa kujeruhiwa wala kupoteza maisha kufuatia tukio hilo.
Katika hatua nyingine, Tume ya Madini imewataka wachimbaji na wananchi kuzingatia kikamilifu taratibu za usalama migodini na kutoa taarifa mapema pindi wanapoona viashiria vya hatari, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.
