NA DIRAMAKINI
KESHO Machi 23,2026 ni Siku ya Hali ya Hewa Duniani, ambapo lengo la siku hii ni kuhamasisha umuhimu wa ufuatiliaji na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa katika kukuza maendeleo endelevu na kulinda maisha ya binadamu.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaambatana na kaulimbiu isemayo: “Pima hali ya hewa leo, ili kesho iwe salama,” inayolenga kusisitiza haja ya kuimarisha mifumo ya uangalizi wa hali ya hewa pamoja na matumizi bora ya takwimu zinazokusanywa.
Kaulimbiu hiyo inaakisi umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi na ya kisayansi katika sekta mbalimbali nyeti za kijamii na kiuchumi.
Aidha, kwa mujibu wa wataalamu wa hali ya hewa, taarifa sahihi na za wakati huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha tahadhari za mapema dhidi ya majanga ya asili, kusaidia shughuli za kilimo, usafiri, nishati pamoja na kulinda miundombinu.
Pia, taarifa hizo ni nyenzo muhimu katika kukuza ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Maadhimisho ya mwaka huu pia yanaadhimisha kumbukizi ya miaka 76 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani mwaka 1950, ambalo limeendelea kuwa mhimili mkuu wa ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya hali ya hewa, maji na tabianchi.
Kwa Tanzania, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaungana na wadau mbalimbali kuadhimisha siku hii kwa kuendelea kutoa huduma za hali ya hewa kwa umma na sekta mbalimbali.
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa,itaendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za hali ya hewa ili kuhakikisha jamii inanufaika ipasavyo na huduma hizo.
Kwa ujumla, Siku ya Hali ya Hewa Duniani ni fursa muhimu ya kukumbusha jamii kuhusu wajibu wa kutumia taarifa za hali ya hewa kwa ufanisi, ili kulinda maisha, mali na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania

