Tanzania na Uganda zasisitiza utekelezaji kwa vitendo katika kukuza ushirikiano wa uwili

DAR-Tanzania na Uganda zimethibitisha tena dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano wa uwili, kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya pamoja, na kuibua maeneo mapya ya ushrikiano.
Akifungua kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kinachofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa idara ya afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ali Bujiku amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Uganda katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Balozi Bujiku alieleza kuwa mkutano huo ni fursa kwa wataalamu wa pande zote kufanya tathmini ya utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa katika JPC ya nne mwaka 2022, kujadili changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, na kupendekeza njia bora za kuimarisha ushirikiano huo.
"Mjadala wetu leo unaakisi upeo mpana na wa kimkakati wa ushirikiano wetu. Tutajadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo diplomasia, ulinzi na usalama, uhamiaji, kilimo, afya, elimu, utamaduni pamoja na biashara.


“Sekta hizi ni muhimu katika kuimarisha uhusiano wa watu kwa watu na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya pamoja,” amesema Balozi Bujiku.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kushughulikia vikwazo vya biashara vinavyoathiri mtiririko wa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Alibainisha kuwa, kuondoa vikwazo hivyo kutasaidia kufungua fursa kubwa za kiuchumi na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, huduma na watu.

Balozi Bujiku pia aligusia umuhimu wa kuboresha miundombinu ya mawasiliano na usafirishaji kati ya Tanzania na Uganda, akitaja miradi ya kimkakati ya kikanda ikiwemo bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki pamoja na barabara na miundombinu mingine ya usafiri ambayo inalenga kuongeza ufanisi wa biashara na kuimarisha ujumuishaji wa kikanda.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa kikao hiki hakilengi tu kupitia tuliyoyafanya, bali pia kuharakisha kasi ya ushirikiano wetu, Wananchi wetu wanatarajia kuona matokeo ya vitendo na hatua za haraka,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali Mstaafu Fred Mwesigye amesisitiza umuhimu wa kutatua changamoto zilizopo na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

“Viongozi wetu wametupa jukumu la kushughulikia masuala haya, watakapokutana tena, tunapaswa kuwa tayari kuwaeleza kwamba tumetatua changamoto zote zilizokuwepo na tumeanzisha maeneo mapya ya ushirikiano,” amesema Balozi Mwesigye.
Balozi Mwesigye pia ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuonesha uongozi madhubuti katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), pamoja na kuteuliwa kwa Mtanzania Balozi Patrick Mbundi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo.Alieleza kuwa hatua hizo zinatoa msukumo mpya katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kukuza maendeleo ya pamoja.

Hii ni JPC ya tano kati ya Tanzania na Uganda JPC ya mwisho ilifanyik a mwaka 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here