Tanzania na Urusi kuimarisha ushirikiano katika teknolojia za kisasa kukuza Diplomasia ya Uchumi

DAR-Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), ameshiriki katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Taasisi ya Innopraktika kutoka nchini Urusi yenye muunganiko wa makampuni zaidi ya 142 ya Teknolojia (High Tech companies) na Kampuni ya Gen Z Corporation Limited ya Tanzania.Hafla hiyo imefanyika tarehe 25 Machi, 2026 katika ofisi ndogo za Wizara zilizopo Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Kombo amesema, Tanzania na Shirikisho la Urusi zimejidhatiti kuimarisha ushirikiano katika teknolojia za kisasa, hatua inayolenga kukuza diplomasia ya uchumi kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi wa pande zote mbili.
Aidha, Mhe. Waziri Kombo amesema hati hiyo ya makubaliano imekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inaendelea kuimarisha utekelezaji wa Sera yake Mpya ya Mambo ya Nje, inayolenga kukuza diplomasia ya uchumi, huku ikisisitiza umuhimu wa teknolojia na ubunifu kama vichocheo vya maendeleo endelevu.

Mhe. Kombo amesema teknolojia ya kisasa ni chachu muhimu katika kupunguza umaskini, kurahisisha upatikanaji wa elimu, masoko ya bidhaa, na huduma za kifedha katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo.

Sambamba na tukio hilo, Mhe. Waziri ameelezea kufurahishwa na pendekezo la makampuni hayo la kuanzisha 'Kituo cha Teknolojia-Technology Hub' nchini Tanzania.

Amebainisha kuwa mpango huo unaendana kikamilifu na azma ya kitaifa ya kuwa kitovu cha teknolojia ya taarifa na mawasiliano (ICT) kikanda.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Innopraktika Bwana Alexander Likhanov amesema Hati hiyo ya Makubaliano ya ushirikiano itahusisha ushirikiano katika teknolojia za kisasa katika kuboresha ufanisi wa kazi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, madini, mawasiliano, usafirishaji na maliasili.

Hafla hiyo imejumuisha wataalam kutoka COSTECH, watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na wajumbe kutoka Kampuni zilizosaini mikataba hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here